Uzinduzi wa tawi la Exim Bank Kahama ni uthibitisho wa
ukuaji wa sekta ya benki, ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali na dhamira
ya kukuza uchumi wa wananchi. Aidha, Serikali imekuwa ikihimiza taasisi za
fedha kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kufanya uwekezaji wa
kimkakati.
Hayo yameelezwa leo Februari 25, 2025 Kahama mkoani
Shinyanga na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
wakati akizindua tawi la Benki ya Exim.
“ Kahama ni kitovu kikubwa cha shughuli za kiuchumi, hasa
sekta ya madini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Zaidi
ya madini, mji huu pia ni maarufu katika sekta ya kilimo na biashara. Ni wazi
kuwa ufanisi wa sekta hizi unategemea upatikanaji wa huduma za kifedha imara na
zinazokidhi mahitaji ya wajasiriamali na wafanyabiashara,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “Hivyo, kwa kufungua tawi hili, Exim Benki inatoa
fursa ya kipekee kwa wakazi wa Kahama kupata huduma za kifedha zinazoendana na
shughuli zao za kiuchumi. Na kunaleta manufaa makubwa kwa jamii ya hapa Kahama,
kwa wateja wengine wa benki na benki yenyewe kwa ujumla,”
Dkt. Biteko ametaja manufaa hayo kuwa ni kuongezeka kwa
fursa za uchumi kwa kuongeza ajira, kuongeza mapato ya benki na hivyo kutumia
sehemu ya faida yake kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia makundi
maalum kadhaa yenye uhitaji yaani (Corporate Social Responsibility - CSR)
Aidha, manufaa mengine ni kuongezeka kwa mapato ya kodi
Serikalini na kuongezeka kwa ushindani wa huduma za kibenki.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza benki hiyo kwa hatua kubwa na
kwa jitihada zake za kuleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi pamoja
na kuiwakilisha Tanzania katika nchi za
Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza Benki ya Exim
kwa kuisaidia jamii kupitia Exim Cares “ Nimefurahi kusikia kuwa kabla ya
kuzindua wa tawi hili tayari mmechangia vifaa vya matibabu katika Hospitali ya
Wilaya ya Kahama vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 25. Mchango huo wa
vifaa vya matibabu utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kahama.
Hatua kama hizi zinaonesha mshikamano wa sekta binafsi na Serikali katika
kuboresha ustawi wa wananchi.”
Pia, amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na
sekta binafsi katika kuimarisha huduma za kifedha na kuhakikisha kuwa
zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi kwa kila Mtanzania.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Benki hiyo kuwashika
mkono na kuwakuza vyema wananchi wa kawaida na wa hali ya chini ambao wao
watakuwa ni wateja muhimu. Aidha, uchumi wa wananchi hao wa kawaida hukuwa kwa
kasi kutokana na shughuli zao za kiuchumi na hivyo kuisaidia pia benki kukua.
Benki hiyo ya Exim inatarajiwa kuwasaidia wananchi wa Kahama
wanaohitaji huduma za kibenki ili kukua kiuchumi kwa kutoa huduma mbalimbali
kama vile fursa za kufungua akaunti, kupata mikopo, na kufanikisha malipo
mbalimbali kwa njia salama na rahisi zaidi.
“ Niwatoe wasiwasi Benki ya Exim kuwa Kahama inafedha na inaendelea kukuwa kwa
sababu ya uwepo wa bandari kavu na katika sekta ya madini mfano Kabanga nikeli
na bidii ya watu wa hapa ya kufanya kazi. Hapa ni soko kubwa na muone fahari
watu wa Kahama wanatajirika kupitia benki yenu,” amemalizia Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi
Macha amesema kuwa ufunguzi wa tawi la benki hiyo ni kielelezo kuwa shughuli za
uchumi ni nyingi na zitaendelea kuimarishwa.
Ameongeza kuwa Mkoa huo una matawi ya benki 11 ambayo yote
pia yapo Kahama hivyo ni kiashiria kuwa
Kahama ipo kibiashara na kuwa Mkoa huo uko tayari kushirikiana na benki hiyo.
Naye, Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara
ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka
mazingira mazuri ya kifedha na kuwa dira iliyopo imekuwa ikiwaongoza na ni
mpango mkuu wa sekta ya fedha ulioandaliwa na Serikali umeweka mazingira
wezeshi na moja ya manufaa yake ni kufunguliwa kwa tawi hilo la benki.
Akitaja idadi ya benki zilizopo nchini amesema kwa sasa kuna
benki 44, matawi zaidi ya 1000 na wakala wa huduma za kibenki zaidi ya 100,000
na hivyo ukuaji wa benki umeongezeka.
“ Wizara tunaipongeza kwa dhati Benki ya Exim kwa kufungua
tawi Kahama na kusogeza huduma hizi karibu na wananchi,” amesema Dkt. Mwamaja.
Pamoja na hayo, amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya
watoa huduma wasio waaminifu na mikopo chechefu, hivyo Wizara kupitia Benki Kuu
imeendelea kukabiliana na changamoto
hizo kwa kutoa elimu ya masuala ya fedha mijini na vijijini ili wananchi
waelewe na kutumia fursa za fedha zilizopo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu
amesema kuwa uzinduzi huo unathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kuleta suluhu
ya masuala ya fedha na uwekezaji ambapo mwaka 1997 walizindua tawi la kwanza
jijini Dar es salaam na kwa sasa taasisi hiyo ina wigo mpana wa kutoa huduma
zake.
“ Benki yetu imekuwa ikishirikiana mwa karibu na watu wa
Kahama kwa shughuli mbalimbali ambapo tumewajulisha wakazi kuhusu huduma zetu
na kuwa mshirika wa kudumu wa fedha,” amesema Bw. Matundu.
Aidha, amesema benki hiyo si tu imesaidia katika sekta ya
afya bali hata elimu, ubunifu na kuwezesha wajasiriamali wanawake.
“Tutaongeza ushiriki wa kifedha kutoka kwa
wafanyabiashara na wananchi wanaotafuta suluhu ya kifedha kwa ajili ya kuongeza
ufanisi katika shughuli zao,” amebainisha Bw. Matundu.




0 Maoni