KATIBU Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amewataka watumishi wa Tume kufanya kazi kwa kujituma na weledi hasa kwenye usimamizi wa shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
Mhandisi Lwamo ametoa rai hiyo mapema leo Februari 25,2025
jijini Dodoma akifungua mafunzo ya matumizi ya mashine maalum za kupima madini
ya metali kwa njia ya Mionzi /X-RAY kwa
watalam wa Tume ya Madini wakiwemo
Wahandisi Migodi, Wahasibu, Watakwimu, Maafisa Utawala na Wataalam wa
Maabara ‘Lab Technologist.
Amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini rekodi ya
makusanyo ya maduhuli ya Serikali imeendelea kukua hali iliyopelekea wadau
wengi wa madini na wananchi kwa ujumla kuwa na taswira chanya ya Tume.
“Mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 tulimaliza kwa kukusanya
Shilingi Bilioni 753, mwaka huu tunatakiwa kukusanya Shilingi Trilioni Moja,
sote tunapaswa kuwa na weledi ili tuweze kufikia lengo, hatuwezi kufika bila
uadilifu, kujituma na kutunza vitendea kazi,”amesema Mhandisi Lwamo.
Katika hatua nyingine,
Mhandisi Lwamo amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea
kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa
Mikoa, Masoko ya Madini, Vituo vya Ununuzi wa Madini na Maabara ikiwa ni pamoja
na upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha na kutatua changamoto zinazowakabili
wachimbaji wa madini nchini.
Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi wanajengewa uwezo wa matumizi sahihi ya mashine za kupima madini ya metali ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia sana kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.




0 Maoni