Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
(Mb) amesema jitihada za Serikali zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii kupitia filamu za
Royal Tour na Amazing Tanzania zimefungua soko la uwindaji wa kitalii Nchini
China.
Mhe. Chana ameyasema hayo jana katika Chuo cha Utalii cha Taifa (NCT) jijini Dar es Salaam
kwenye Hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii
kwa wawekezaji mbalimbali kutoka Makampuni ya K&F Wild Expedition Limited, Michael Mantheakis
Safaris Limited, Out of Africa Safaris Limited na Royal Conservation Limited.
"Nichukue fursa hii kuwapongeza makampuni yote kwa
kushinda vitalu hivi vya uwindaji wa kitalii sambamba na hilo nichukue fursa hii kumpongeza mwekezaji
kutoka Nchini China kwa kupitia kampuni ya K&F Wild Expedition Ltd kwa kuwa
kampuni ya kwanza ya kutoka China kuwekeza katika vitalu vya uwindaji wa
kitalii nchini," amesema Mhe. Chana.
Mhe. Chana ameongeza kuwa soko la uwindaji wa kitalii nchini
China linakua kwa kasi na yote haya ni kwa kupitia jitihada zinazofanywa na
Serikali za kutangaza utalii duniani.
Sambamba na utoaji wa vyeti kwa wawekezaji, Mhe. Chana alishuhudia
zoezi la utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment
Concessions Areas- SWICA) kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA) na Kampuni ya Neon Investment Limited.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA,
Mej. Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema kuwa TAWA inaendelea kutumia mbinu
mbalimbali za kuvutia wawekezaji ikijumuisha matumizi ya mnada wa kielektroniki
wa ugawaji wa vitalu.
Sanjari na hilo, Mej.Jen (Mstaafu) Semfuko ameongeza kuwa Bodi
ya Wakurugenzi itaendelea kutafuta masoko mengine ya uwindaji wa kitalii
yakiwemo nchi za China, Urusi, Uturuki, Brazil na Mashariki ya Mbali ili
kuhakikisha wawekezaji wanaongezeka na Nchi inaendelea kupata mapato.
Naye, Kaimu Kamishna wa TAWA Mlage Kabange, amesema kupitia
uwekezaji huu Serikali inatarajia kupokea mapato na tozo mbalimbali.
"Kupitia ada za vitalu za makampuni haya Serikali
inatarajia kupata mapato takribani shilingi za kitanzania Bilioni 2.5 kwa mwaka
mbali na kodi nyingine."
Sambamba na hilo, Kaimu Kamishna Kabange amesema kuwa uwekezaji huu unawagusa pia wananchi wanaoishi pembezoni ya hifadhi kwa kuzingatia kuwa kwenye mikataba hii kuna kipengela mahsusi cha kunufaisha jamii zinazoishi pembeni mwa hifadhi.




0 Maoni