SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Mamlaka ya
Hali ya Hewa nchini ikiwemo upande wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na
kujenga uwezo wa wafanyakazi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo
(Jumanne, Januari 21, 2025) alipozindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF) - Project” katika
Ukumbi wa Hotel ya Midland Inn View, Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali la
kuendelea kufanya maboresho hayo ni kuwezesha utoaji wa utabiri wa hali ya hewa
na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
Amesema miongoni mwa uwekezaji huo ni ununuzi wa rada
saba za hali ya hewa, upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na uboreshaji
wa vifaa vya hali ya hewa kwa kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki kwa mujibu wa
matakwa ya Mkataba wa Minamata.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ya Tanzania katika kuunga
mkono utekelezaji wa mradi wa SOFF imetenga fedha za kununua Vituo 11 vya Hali
ya Hewa. Vituo hivyo vinavyojiendesha vyenyewe vitachangia data katika Mtandao
wa Kimataifa wa Uangazi.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaunga mkono kwa kutoa
mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni nne ambazo ni thamani ya mchango
kwa njia ya huduma zisizo za kifedha (In-Kind contribution). “Jitihada zote
hizo, zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya
hali ya hewa.”
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mradi wa SOFF “SOFF -
Investment Phase Project”, Mheshimiwa Majaliwa amesema mradi huo una umuhimu
mkubwa siyo tu kwa kukidhi mahitaji ya data za hali ya hewa na tabianchi kwa
ajili ya utabiri wa hali ya hewa duniani, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na
ubadilishanaji data za hali ya hewa kimataifa, hivyo kuimarisha huduma za hali
ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa. “Mafanikio katika utekelezaji
wa SOFF yatachangia sana kuimarisha ustahimilivu wa matukio ya hali mbaya ya
hewa kwa maendeleo endelevu nchini”.
Amesema kuwa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea
unategemea sana sekta zinazohusiana moja kwa moja na hali ya hewa, ambazo ni
kilimo, lakini pia, ufugaji, nishati, maji, afya, madini na usafirishaji.



0 Maoni