Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 521 katika kipindi cha Julai 1, 2024, hadi Desemba 31, 2024. Hii ni sawa na asilimia 52.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde, leo Januari 21, 2025, jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya
utekelezaji ya Wizara mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Waziri Mavunde amesema mafanikio hayo yanatokana na
usimamizi mzuri, udhibiti madhubuti, na weledi katika ukusanyaji wa mapato
kwenye sekta ya madini.
“Wizara imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mwaka wa
fedha wa 2015/16 ambapo ilikusanya shilingi bilioni 161 kwa mwaka mzima na
mwaka huu ndani ya nusu ya kwanza tayari
tumekusanya asilimia 52.2 ya lengo la Shilingi trilioni 1 kwa Mwaka wa Fedha wa
2024/25,”
STAMICO Yapiga Hatua Kubwa
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameongeza kuwa
leseni kubwa na za kati za madini ambazo hazijaendelezwa zitarudishwa
Serikalini zitakabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kwa ajili ya
kuziendeleza kwa manufaa ya taifa.
Aidha, Mhe. Mavunde amesema kuwa, STAMICO imejipanga kuwa
sehemu muhimu ya uzalishaji wa Madini ya Kinywe hapa nchini ikiwa ni sehemu ya
juhudi za Tanzania kuwa kiungo muhimu katika soko la dunia la madini hayo.
Pia, Waziri Mavunde amefafanua kuwa, katika juhudi za
Serikali kuwasaidia wakulima wa chumvi nchini, STAMICO itajenga kiwanda kikubwa
cha kusafisha chumvi Mkoani Lindi ili kuimarisha soko la wakulima hao na kwa
Mitambo ya kiwanda hicho imeshawasili nchini na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi
Februari 2025.
Utafiti wa Madini wa Kina Kuimarika
Waziri Mavunde amesema, kupitia Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Wizara imegawa nchi katika vitalu sita vya
utafiti. Katika mwaka huu wa fedha, asilimia 18 ya nchi itafanyiwa utafiti wa
kina ili kuongeza kanzidata ya maeneo yenye madini na kuvutia uwekezaji zaidi.
Pongezi kwa Wizara ya Madini
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Mathayo David, amepongeza juhudi za Wizara ya
Madini katika ukusanyaji wa maduhuli na kuimarisha Sekta hiyo.
Vilevile, Mhe. Dkt. Mathayo amepongeza pia uteuzi wa
Mhandisi Ramadhani Lwamo kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, akimtaka
kutekeleza majukumu yake kwa weledi na bidii ili kudumisha uaminifu wa Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mnada wa Madini ya Vito Mirerani
Awali, akizungumzia mnada wa madini ya vito uliofanyika
Desemba 14, 2024, katika Mji Mdogo wa Mirerani, Mkurugenzi wa Sera na Mipango
wa Wizara ya Madini, Augustine Olal, amesema kuwa washindi wa zabuni 47 waliuza
madini yenye thamani ya shilingi bilioni 1.13. Serikali ilipata shilingi
milioni 80 kama mapato.
Ikiumbukwe kuwa , Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya
shilingi trilioni 1 katika Mwaka huu wa Fedha 2024/25. Aidha, Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
inaelekeza Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa kufikia
mwaka 2025.

0 Maoni