Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amezindua
rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, tarehe
21 Januari, 2025 katika Ukumbi Mkubwa wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro,
Uzinduzi huo, utafuatiwa na Kliniki ya Sheria bila malipo
kwa wananchi inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro. Huduma hizi
zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi
Moshi Mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 21 hadi 27 Januari 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Kliniki hiyo Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro na kuja kutoa
huduma ya Kliniki bure kwa wananchi wa Kilimanjaro.
"Tunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa kuja kutoa huduma hii bure kwa wananchi wetu hii inaonyesha namna Ofisi hii
ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini,"amesema
Mhe. Babu.
Aidha, Mhe. Mkuu wa mkoa ameeleza kuwa Kliniki hiyo
itasaidia kupunguza migogoro ya Wanachi dhidi ya Serikali, zitawezesha Mawakili
wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria, pia zitawasaidia Mawakili wa Serikali
kushirikiana kwa ukaribu na Wadau pamoja Wananchi katika kutatua masuala ya
Kisheria.
"Leo
tunakwenda kuanza Kliniki ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi
wenye matatizo ya kisheria, kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali itakuwa inatatua changamoto mbalimbali za wananchi". Amesema Mhe.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ametoa
wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kushiriki kwa wingi katika Kliniki hiyo ili
wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Bi. Tamari Mndeme amesema Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za Kisheria bure kwa
wananchi kupitia Kliniki hiyo.
"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari
kuwahudumia Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha
tunaamini kupitia Kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa,"
amesema Bi. Tamari.
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa
Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika
kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.



0 Maoni