WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amewataka wazazi wahakikishe
wanawaandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule badala ya kuwaacha
wakauze maandazi, karanga na miwa.
Amewataka watendaji wa kata kote nchini wakae na
watendaji wa vijiji na mitaa ili kuwahimiza suala la uandikishaji wa watoto
wenye umri wa kwenda shule. “Mtoto wa Kitanzania anatakiwa kwenda shule, kwa
sababu mtoto huyu leo ameandaliwa utaratibu wa kuanzia chekekea, shule za msingi
hadi sekondari. Tunahitaji kuona watoto wa Busega wakienda shule wote,”
amesisitiza.
“Niwasihi wazazi, fuatilieni mahudhurio ya watoto wenu
ili kubaini kama kweli wanaenda shule na wanasoma. Wanaporudi nyumbani, kagueni
madaftari yao ili kuona wamejifunza nini. Zaidi ya hayo, muwasimamie watoto wa
kike ili wahitimu masomo yao bila kubughudhiwa,” amesisitiza.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Desemba 22, 2024) wakati
akizungumza na maelfu ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya ya
Busega, uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Lion of Judah,
wilayani Busega, mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
amewekeza sana kwenye upatikanaji wa elimu nchini kwa kutoa fedha ya ujenzi wa
shule, madarasa na mabweni. “Pia ametoa fedha za elimu bila ada ili kuhakikisha
kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya elimu.”
Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri Mkuu
amesema umefika wakati sasa taasisi zenye watu zaidi ya 100 zianze kutumia
nishati hiyo huku akiwakumbusha wadau kuwa ukomo wa matumizi ya nishati chafu
ni Desemba 31, mwaka huu.
“Wananchi mmoja waanze taratibu kuachana na matumizi ya
nishati chafu kwa kubadilisha teknolojia. Tuhame kutoka kwenye kuni na mkaa na
tuanze kutumia nishati ya gesi, umeme na aina nyingine ya mkaa ambao
unatenegenezwa kwa kutumia takataka.”
Ametumia fursa hiyo kuwaelezea wajumbe wa mkutano huo,
mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Fedha nyingi zimetolewa kwenye sekta ya elimu ambazo
zimetumika kujenga miundombinu ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati
(VETA) pamoja na ukarabati mkubwa wa vyuo vikuu.”
Kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu amesema zimetolewa
fedha nyingi kujenga vituo vya afya, hospitali za wilaya na za halmashauri
zenye hadhi ya hospitali za wilaya pamoja na ujenzi wa hospitali za kanda.
Kuhusu umeme, Waziri Mkuu amesema: “Vijiji vyote vya mkoa
huo vimepata umeme, imebakia tu kazi ya wananchi kuuvuta. Leo hii tunaenda
kwenye ngazi ya vitongoji na kupeleka umeme kwenye visiwa, iwe ni umeme wa jua
au wa kupitisha kwenye bomba chini ya maji kwenda kwenye kisiwa kama cha
Ukerewe.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema utulivu uliopo
kwenye wilaya ya Busega unatokana na sera za CCM ambazo zinatabirika tangu enzi
za waasisi wa Taifa hili. “Mshikamano na utulivu, uwepo wa maadili ni utamaduni
wa Taifa letu na hata matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamedhihirisha
imani waliyonayo wananchi kwa Chama cha Mapinduzi.”
Mapema, Mbunge wa Busega, Simon Songe kwa kuwezesha
upatikanaji wa huduma nyingi za kijamii kwenye wilaya hiyo ndani ya muda mfupi.
“Watu wa Busega tuna imani sana na Serikali ya awamu ya sita, maendeleo
yaliyofanyika ni makubwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa. Tuna imani kuwa
itakamilika mapema ili wakazi wa Busega waweze kwenda Dar es Salaam chini ya
saa sita,” amesema.
Ameishukuru Serikali kwa kutoa sh. bilioni 19.9 ambazo
katika kipindi cha Desemba 2020 hadi Oktoba 2024, zimewezesha utekelezaji wa
miradi kadhaa ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa, vyoo
na madawati.
“Mradi wa VETA utakaogharimu shilingi bilioni 1.484
tayari umeshaanza kujengwa na ninaamini mwaka 2026 utakuwa umekamilika na
wananchi wataanza kuitumia. Tunamshukuru sana Mhe. Rais na Serikali ya awamu ya
sita kwa uwekezaji huu muhimu kwa maendeleo ya vijana wetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi
alisema mkoa huo umepokea sh. bilioni 858.5 ambazo zimetumika kuboresha sekta
za elimu, afya, maji na umeme.
Aliishukuru Serikali kwa kupeleka magari ya wagonjwa
manne, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaogharimu sh. bilioni 440 na
ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kwa gharama ya sh. bilioni 97.
0 Maoni