WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Wakala
ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza waongeze kasi ya ujenzi wa
daraja la Simiyu lililoko wilayani Magu kwenye barabara kuu ya Mwanza-Musoma
ili likamilike kwa wakati.
Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 175, upana wa
mita 12.3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa tatu, ulianza Oktoba
30, 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 29, 2025. Daraja hilo linaunganisha
mikoa ya Mwanza na Mara.
Akizungumza na wananchi waliofika kwenye daraja hilo jana
jioni (Jumamosi, Desemba 21, 2024), Waziri Mkuu alisema wilaya ya Magu ina
fursa nyingi za kiuchumi na kukamilika kwa ujenzi huo, kutafungua milango kwa
wana-Magu.
“Magu ni wilaya ya fursa kiuchumi, Magu ni pumulio la
Jiji la Mwanza. Je wana-Magu mmejipangaje kuzikamata hizo fursa? Ninawasihi
jengeni vituo vya mabasi, mahoteli, maeneo ya vyakula na burudani. Boresheni
miundombinu ya usafirishaji ili mtu akitoka Mwanza awe na uhakika kuwa anaweza
kurudi kwa haraka bila shida yoyote.”
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa daraja
hilo, Mhandisi Katetula Kaswaga kutoka TANROADS Makao Makuu alisema mradi huo
utakaogharimu sh. bilioni 48.7, unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.
“Mradi unajengwa na mkandarasi China Civil Engineering
Construction Corporation (CCECC) chini ya usimamizi wa mhandisi mshauri ambaye
ni TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU). Kazi iliyofanyika hadi sasa
imefikia asilimia 35,” alisema.
Mapema, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey
Kasekenya amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo, kutasaidia
kupunguza ajali na msongamano kwa kiasi kikubwa kwani daraja la zamani lilikuwa
na njia moja ila la sasa litakuwa na njia mbili.
Amesema ujenzi wa daraja la Simiyu ni miongoni mwa miradi
mikubwa nchini ambayo imelenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi. “Daraja hili
lilijengwa kabla ya uhuru, lilikuwa limebakia peke yake kwenye barabara kuu za
nchi nzima.”
“Serikali ya awamu ya sita ilishaamua kuondoa madaraja
kama hayo kwenye barabara kuu nchini. Tungeliacha liendelee kuwepo, lingeleta
changamoto ya foleni kwenye magari ya mizigo yanayokuja nchini na kwenda kupita
kwenye daraja la Kigongo-Busisi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi
la ujenzi wa daraja la Sukuma katika kata ya Ng’haya ambalo linaunganisha
wilaya za Magu na Bariadi.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 70, upana wa mita 11.3 na
barabara unganishi za kilomita 2.3, linajengwa na mkandarasi mzawa ambaye ni
Mumangi Construction Co. Ltd. Hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 24 na
utagharimu sh. bilioni 10 hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey
Kasekenya alisema ujenzi wa daraja hilo ni utekelezaji wa moja ya mikakati ya
Serikali ya kuboresha sekta ya miundombinu nchini na kwamba kukamilika kwa
daraja hilo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, na pia
kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.
Alisema daraja litakapokamilika na barabara hiyo ikaanza
kutumika, itafupisha safari za kwenda mkoani Mara. “Barabara hii itakuwa fupi
sana, ni kilometa 74 tu kwenda Mara,” alisema.
Kwenye ziara hiyo ya siku moja, Waziri Mkuu alifuatana na
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey
Kasekenya, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba, Wabunge wa Magu,
Sengerema, viti maalum na viongozi wa CCM mkoa wa Mwanza.
0 Maoni