Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Hazara
Chana (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan amemvisha cheo na kumuapisha Dkt. Elirehema J. Doriye Kuwa
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Akimuapisha Dkt Doriye katika hafla iliyofanyika leo
tarehe 23 Desemba, 2024 katika viwanja vya makao makuu ya NCAA, Waziri Balozi
Pindi Chana amempongeza Dkt Dorie kwa kusimamia ongezeko la mapato ambapo
katika kipindi cha mwezi Julai hadi
Novemba, 2024 jumla ya shilingi Bilioni
138,680,341,953.65 zimekusanywa huku
watalii 551,512 (Watalii wa nje 350,091 na watalii wa ndani 201,421)
wakitembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika kipindi cha miezi mitano.
“Nakupongeza kwa juhudi hizi kubwa ulizozifanya katika
kipindi cha miezi minne iliyopita, endelea kuongeza juhudi katika usimamizi wa
mapato, kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),
kuimarisha Mahusiano ya kikazi, Usimamizi wa haki za watumishi, mahusiano na
wadau na kuongeza hamasa ya Utalii wa ndani ” aliongeza Balozi Chana.
Mwenyekiti wa bodi ya wakurunezi wa NCAA, Jenerali
Venance Mabeyo (Mstaafu) amempongeza Dkt Doriye kwa kuteuliwa, kuvishwa cheo,
kuapishwa na kumuomba kuendelea
kusimamia kikamilifu shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa
kuzingatia misingi ya weledi, uzalendo, uvumilivu na kumsisitiza kuishi katika
kiapo alichoapa katika kuanza majukumu mapya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan
Abbasi amempongeza Dkt Doriye kwa uteuzi, kuhudhuria mafunzo ya jeshi la
Uhifadhi na kuhitimu hivi karibuni na kumuwezesha kuvalishwa cheo na kuapishwa na kuwataka watumishi wa NCAA kutoa
ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Akitoa shukrani baada ya kuapishwa, Kamishna wa
Uhifahifadhi NCAA ametoa vipaumbele vyake katika utendaji kazi kuwa atajikita
katika Kusimamia Uhifadhi Endelevu, Kukuza Utalii wa Kimkakati, Ushirikiano na
Jamii, Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi, kukabiliana na Changamoto kwa Ufanisi
hasa katika kutumia changamoto kama fursa ya kujifunza na kuboresha utendaji
kazi.
Hafla ya uapisho na uvalishwaji cheo kwa kamishna wa uhifadhi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Lucas Kitandula, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Wakurugenzi NCAA, Wakuu wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Katibu tawala Mkoa wa Arusha, wawakilishi wakuu wa Wilaya za Karatu na Ngorongoro pamoja na wageni wa makundi mbalimbali.
Na. Kassim Nyaki- Karatu
0 Maoni