Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu Bw. Amos Nnko amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea
maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo iliyotokea siku ya Jumapili, Desemba 22, 2024
majira ya mchana, pia ilipelekea kifo cha binti yake wa kwanza, Maureen Nnko.
Pia katika ajali hiyo, mke wa marehemu Bi. Agnes Nnko na
watoto Marilyn, Melvin na mwanafamilia mwingine, Sylvana, walijeruhiwa.
Majeruhi wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya
KCMC na Mawenzi.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu Jumatatu, Desemba 23,
alisema kifo cha Bw. Nnko ni pigo kubwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taifa
kwa ujumla.
Bw. Mchechu alimuelezea marehemu Nnko kama mchapakazi,
muadilifu na mtu wa watu.
“Tumepokea taarifa za kifo cha Nnko kwa masikitiko
makubwa sana. Tumepoteza nguzo muhimu,” alisema Bw. Mchechu.
Sanjari na hilo, Bw. Mchechu alitoa pole kwa familia ya marehemu huku
akiwaombea majeruhi wa ajali hiyo uponyaji wa haraka.
Bw Mchechu alisema taratibu za mazishi zinaendelea
kuratibiwa huko Tengeru, Arusha kwa ushirikiano wa familia ya marehemu na Ofisi
ya Msajili wa Hazina.
0 Maoni