Timu ya Nyabiyonza ya Karagwe mkoani Kagera imeibuka
kidedea kwa kuifunga mabao mawili kwa moja timu ya Nyuki FC kutoka Bukombe,
mkoani Geita katika mechi ya kirafiki iliyofanyika katika Uwanja wa Bashungwa,
Karagwe mkoani Kagera.
Akizungumza jana Desemba 20, 2024, Karagwe mkoani Kagera
mara baada ya mtanange huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri na Nishati, Mhe. Dkt.
Doto Biteko amewapongeza washiriki wa mechi hiyo na kusema mchezo huo ni sehemu
ya kuimarisha umoja, upendo na amani iliyopo.
“Nataka niwahakikishie kuwa watu wa Bukombe watatoka hapa
wakiamini ni washindi wa pili, nawapongeza sana makocha wa timu hizi mbili na
waamuzi kwa kuamua mpira kwa haki,” amesema Dkt. Biteko.
Pia, amewaasa wananchi wa Karagwe kuishi kwa upendo “
Nataka niwasihi watu wa Karagwe kuimarisha umoja wenu kupendana na kuimarisha
amani ya wilaya hii.”
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha
Mkoa wa Kagera unapata maendeleo hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea
kudumisha amani iliyopo ili kuchochea maendeleo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa
amefurahishwa na matokeo ya mechi hiyo ya kirafiki kutoka Wilaya ya Bukombe na
Karagwe kuisha salama na kuwapongeza wachezaji.
Amesema kuwa mechi hiyo ya kirafiki ilikuwa wazo la Dkt.
Biteko mara baada ya timu ya Nyuki kushinda fainali katika mashindano ya ligi
ya KNK (Kusema na Kutenda).
“Nilipokuja Bukombe kwenye fainali ya KNK Cup
ulinielekeza baada ya vijana kushinda fainali
ile sasa waje kucheza mechi ya kirafiki Karagwe. Kwa niaba ya wananchi
wa Karagwe na Bukombe nakushukuru sana kwa wazo lako ambapo leo limeweza kuleta
burudani nzuri kupitia mechi hii,” amesema Mhe. Bashungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amewashukuru
Dkt. Biteko na Mhe. Bashungwa kwa kuandaa timu hizo zilizoleta burudani kwa
wakazi wa Karagwe.
Mabingwa wa mechi hiyo timu ya Nyabiyonza imenyakua
kitita cha kiasi cha shilingi milioni sita, seti moja ya jezi, mpira na kombe
wakati mshindi wa pili Nyuki FC akiondoka na kitita cha fedha shilingi milioni
nne, seti moja ya jezi na mpira.
Lazaro Peter wa Nyuki FC ameibuka mchezaji bora wa mechi
zote mbili huku mlinda mlango bora wa mechi hizo akiwa Rena Mwameja wa
Nyabiyonza FC.
0 Maoni