Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa
watatu kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara ya madini Peter Bruno Mteta (59)
mkazi wa Matundasi Wilayani Chunya.
Kamanda wa Polisi Mbeya SACP Benjamin
Kuzaga ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 12, 2024 saa 2:00 usiku kwa kumpiga
risasi mgongoni mfanyabiashara huyo akiwa nyumbani kwake.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Kenedy
Richard maarufu Majiulaya (26) mkazi wa Kijiji cha Galula Wilaya ya Songwe
mkoani Songwe, Msafiri Peter Mwahonje maarufu Wakwetu (48) mkazi wa Matundasi na
Uhuru Ulaya Sukwa (63) mkazi wa Magamba Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe.
SACP Kuzaga amesema baada ya tukio hilo,
Jeshi la Polisi lilianza upelelezi wa na Novemba 01, 2024 Kijiji cha Ubaruku
Wilaya ya Mbaralimkoani Mbeya watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusiana na tukio hilo
wakiwa na silaha iliyotumika katika tukio hilo pamoja na risasi zake tano.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi
linamshikilia Hamis Shizya Kasunga (50) mkazi wa Maghorofani Jijini Mbeya kwa
tuhuma za kumuua mke wake aitwaye Emmy Fred Mwasile (35) mkazi wa Forest
Maghorofani Jijini Mbeya kwa kumpiga kwa kitu kizito sehemu mbalimbali za mwili
wake.
Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa tukio lililotokea
Novemba 20, 2024 saa 6:30 mchana huko Mtaa wa Foresy mpya, Jijini Mbeya
kutokana na wivu wa mapenzi akimtuhumu mke wake kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine.
Amesema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia
na katika ufuatiliaji alikamatwa Novemba 23, 2024 saa 9:00 alasiri katika mji mdogo
wa Tunduma Mkoani Songwe akiwa katika harakati za kuvuka mpaka kwenda nchini
Zambia.
0 Maoni