Kikao cha Kamati ya Pamoja cha
Wataalamu wa Tanzania na Uganda (JTC) kimeanza mkoani Kagera nchini Tanzania
kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.
Kikao hicho kimeanza leo tarehe 5
Novemba 2024 na kutarajiwa kumalizika Novemba 7, 2024
kinafanyika katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kuhusisha
wataalamu kutoka nchi za Tanzania na Uganda.
Akifungua kikao hicho cha siku tatu kwa
niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat
Fatma Abuubakar Mwasa, katibu Tawala
mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki
amesema, Tanzania imejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi la uimarishaji mpaka
wa kimataifa kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo mbili.
Amebainisha kuwa, uimarishaji mpaka wa
kimataifa kati ya Tanzania na Uganda una lengo la kuweka usimamizi mzuri wa
mpaka baina ya nchi hizo pamoja na kukuza amani, upendo, usalama na maisha ya
watu wake.
Kupitia hotuba hiyo ya Mkuu wa mkoa wa
Kagera, Bw. Ndaki amesema, Tanzania na Uganda zimekuwa na mahusiano mazuri
ikiwemo tamaduni zinazofanana alizozieleza kuwa, zimewezesha wananchi wa nchi
hizo mbili kuishi kwa upendo.
"Ni imani yangu kila mshiriki
katika kikao hiki atatumia muda kuhakikisha uimarishaji mpaka wa kimataifa
baina ya nchi zetu unakuwa na matokeo mazuri kwa ustawi wa nchi na wananchi
wetu," amesema.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
ambaye ni mkuu wa timu ya Tanzania katika kikao hicho Bw. Hamdouny
Mansoor amesema, mkutano huo ni utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika kuhusu
uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa nchi za Afrika kufikia mwaka 2027.
"Ni nia ya Umoja wa Afrika kuzifanya nchi
za Afrika kuwa na amani pasipo migongano wakati wa zoezi zima za uimarishaji
mipaka ya kimataifa," amesema Mansoor.
Kwa upande wake Mkuu wa ujumbe wa timu
ya wataalamu kutoka Uganda Bi. Jacqueline Banana Wabyona ameihakikishia
Tanzania ushiriki mzuri kwenye kikao hicho kwa lengo la kufikia matokeo chanya
ya uimarishaji mpaka kati ya Tanzania na Uganda.
Mpaka wa Tanzania na Uganda una urefu
wa takriban km 397.8 ambapo kati ya hizo km109 ni nchi kavu, km 42.8 ni sehemu
ya Mto Kagera na km 246 ni sehemu ya Ziwa Victoria.
Zoezi la uimarishaji mipaka ya
kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka
2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.
Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo
ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na
Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu
mbili za nchi kavu na majini.
Na. Munir Shemweta- WANMM Bukoba
0 Maoni