Imeelezwa kwamba katika kuendeleza
shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini na kuhakikisha rasilimali madini
zinaongoza kuchangia katika Pato la Taifa, wizara na taasisi zake zinaendelea
kutekeleza mikakati na mipango kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 15, 2024
na Waziri na Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akitoa ufafanuzi juu ya hoja
mbalibali zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
jijini Dodoma.
Akielezea kuhusu mikakati iliyopo
ndani ya wizara kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025, Waziri Mavunde amesema kuwa,
katika kuimarisha uchimbaji wenye tija na uhakika serikali itajenga maabara ya
kisasa mkoani Dodoma na Geita ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupeleka
sampuli zao kwa uchunguzi.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa, wizara
itaendelea kutumia mpango wa ushirikiano baina ya taasisi za Umma na taasisi za
sekta binafsi katika kuendeleza miundombinu ya barabara na nishati ya umeme
sehemu zenye uchimbaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
madini Dkt. Steven Kiruswa ameeleza
kuwa, elimu kuhusu tozo zinazotozwa, wajibu wa mmiliki wa leseni kwa jamii ,
ushiriki wa watanzania katika uvunaji wa rasilimali madini na utunzaji azingira
katika shughuli za uchimbaji ilitolewa kwa wachimbaji wadogo katika Kamati za
Maendeleo za Kata.
Awali, akiwalisha taarifa kuhusu
mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwasogezea huduma za Ugani
katika mkoa wa Dodoma kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kamishna wa
Madini Dkt. AbdulhRaman Mwanga amesema, wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu
matumizi salama ya zebaki katika wilaya ya Chamwino na Bahi.
Sambamba na hapo Dkt. Mwanga amesema,
wizara itaendelea kuboresha mifumo ya utoaji na usimamizi wa leseni za madini
pamoja na kuwezesha utafutaji wa madini kwa njia ya uchorongaji.
Mikakati mingine ni pamoja na kutoa
elimu kuhusu athari za mazingira zitokanazo na uchimbaji wa madini ujenzi,
elimu kuhusu tozo za madini na haki madini katika wilayani ya Dodoma na
vitongoji vyake.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati wa Kamati
ya Bunge Nishati na Madini Dkt.David Mathayo David, ameipongeza wizara kwa
juhudi mbalimbali inazofanya katika mnyororo mzima wa thamani madini kutoka
asilimia 7.1 mpaka kufikia asilimia 9
katika kuchangia Pato la Taifa.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi
ya Mwaka 2022, mkoa wa Dodoma una jumla ya watu 260,505 wanajihusisha na
shughuli mbalimbali kwenye mnyororo wa
thamani wa uchimbaji mdogo ambapo kati ya hao wanaume ni 126,841 na wanawake ni
133,664 ambayo sawa na asilimia 4.6 ya watu wote wanaojishughulisha na shughuli
hizo nchini.
Na. Samwel Mtuwa- Dodoma
0 Maoni