Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema
kufuatia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo
inayowakabili wananchi hasa katika mikoa ya Ruvuma na Lindi, Serikali kupitia TAWA
imetenga bajeti kwa ajili ya kununua ndege nyuki nne (4) aina ya DJI Mavic 3
ambazo zitapelekwa katika wilaya za Namtumbo (Ruvuma) na Liwale, Nachingwea na
Lindi mkoani Lindi.
Kamishna Mabula ameyasema hayo jana Oktoba 15, 2024 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati
wa ziara ya kufuatilia utakelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa Mkoani humo Septemba
28, 2024 kuhusu udhibiti wa wanyamapori
wakali na waharibifu katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.
Sambamba na hilo, Mabula amesema
katika mwaka wa fedha 2024/25 TAWA inatarajia kuajiri Askari 351 ambao
watapangiwa vituo vilivyopo kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyamapori
hao ambapo Askari 20 watapangiwa katika kituo kidogo cha Songea na watafanya
kazi katika wilaya za Tunduru na Namtumbo, wilaya zinazotajwa kuwa na
changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Vilevile, Kamishna Mabula amesisitiza
kuwa TAWA inatarajia kununua gari moja (1) na pikipiki mbili (2) ambavyo
vitapelekwa kituo kidogo cha Songea na vitatumika Katika kudhibiti changamoto
ya wanyamapori hao katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.
Pia, Mamlaka itaboresha kituo kimoja
cha Askari cha kudumu katika wilaya ya Tunduru na vikosi viwili vya kudumu vya
Askari kutokea kituo kidogo cha Songea ili kurahisisha mwitikio wa haraka wa
matukio ya tembo.
Kamishna Mabula ameongeza kusema kuwa
baada ya changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuendelea kuonekana
inakuwa kubwa, Wizara ya Maliasili na Utalii iliandaa Mkakati wa kukabiliana na
migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu ambao
unatekelezwa na Taasisi za Wizara zilizo chini ya Jeshi la Uhifadhi wa
Wanyamapori na Misitu (TAWA , TANAPA, NCAA na TFS) kwa kugawana maeneo,
Halmashauri za Wilaya, Taasisi zisizo za kiserikali, wadau wa Uhifadhi na
wananchi kwa ujumla.
Aidha, katika hatua nyingine kutokana
na uwepo wa bustani ya wanyamapori hai inayosimamiwa na TAWA (Ruhila Zoo)
katika Manispaa ya Songea, bustani inayotajwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa
wakazi wa Mkoa huo, Kamishna Mabula amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma
Kanali Ahmed Abbas Ahmed kusaidia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye
urefu wa Kilometa 5 ambayo itafika moja kwa moja katika bustani hiyo ili
kuwawezesha wakazi wa Mkoa huo kufika kirahisi katika kivutio hicho cha utalii.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Kanali Ahmed Abbas Ahmed amempongeza Kamishna huyo kwa hatua za haraka
alizochukua za kufuatilia utakelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia maelekezo aliyoyatoa
alipokuwa katika ziara yake mkoani humo mwezi Septemba, 2024.
Kanali Ahmed Abbas Ahmed pia
ameipongeza TAWA kwa jitihada walizochukua kama mipango ya muda mfupi na muda
mrefu katika kukabiliana na changamoto hiyo mkoani humo na kukiri kuwa jitihada
hizo zinarudisha matumaini kwa wananchi wa Ruvuma kwa kuwa zinalenga kuimarisha
usalama wa maisha na mali zao dhidi ya uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo ya
wananchi hao.
Na. Beatus Maganja- Ruvuma
0 Maoni