Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezielekeza Halmashauri zote nchini kuzuia
mianya inayosababisha moto kwenye maeneo ya misitu huku akisisitiza matumizi ya
Sheria ndogo za Misitu.
Ameyasema hayo leo Oktoba 8, 2024
katika kikao kilichofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.
"Kila kikao cha Serikali ya
kijiji ajenda ya kudhibiti moto iwe ya kudumu na ninashauri kamati ya kudhibiti
matukio ya uchomaji moto iwe mpaka kwenye ngazi ya kijiji au kata,"
amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, amesisitiza kuhusu kufanya
ulinzi shirikishi ili kujua waanzilishi wa moto sambamba na kufanya tafiti za
miti inayofaa kwa mkaa ili wananchi wapewe vibali vya kuipanda waachane na
uchomaji misitu.
Awali, akiwasilisha taarifa ya matukio
ya uchomaji moto ovyo Wilayani Makete
kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2024/2025, Afisa Misitu, George Africanus alisema kuwa
jumla ya eneo lenye ukubwa wa ekari 1960 zimeungua kwa moto zenye thamani ya
shilingi bilioni 1.4.
Amefafanua kuwa moto huo ulitokea
katika kata za Mbalatse, Mang'oto na
Matamba ambapo moto huo umeunguza miti ya kupandwa, miti ya asili,
mashamba na nyasi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma
Samwel Sweda amesema Halmashauri inaendelea na zoezi la kuelimisha wananchi juu
ya umuhimu wa kuacha kuchoma misitu na kuunda Kamati za kudhibiti moto.
Na. Happiness Shayo- Makete
0 Maoni