Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Matengenezo ya Barabara wa Sierra Leone Bw. Mohamed Kallon ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa madaraja na barabara kwa kutumia mawe.
Akizungumza na waandishi wa habari
Mtendaji Mkuu huyo amesema wamefurahishwa na teknolojia hiyo ambayo kwa kiasi
kikubwa inapunguza gharama za ujenzi pia kutumia malighafi zilizopo eneo
husika.
Amesema kwamba ujio wao hapa nchini ni
kujifunza ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya katika maeneo ya mipango,
ushirikishwaji wa wananchi na utumiaji wa teknolojia mbadala.
“Wananchi wa Sierra Leone ni
wazalishaji na wengi wanaishi vijijini hivyo kwa kutumia teknolojia ya mawe
itawarahisishia kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko.”
Ameongeza kusema kuwa kati ya agenda
tano za Rais wa nchi yao ni kuilisha Sierra Leone hivyo kitu muhimu ni kufungua
barabara ili kuuza na kusafirisha mazao toka kwa wakulima.
Kwa upande wa ushirikishwaji wa
wananchi (vikundi vya kijamii) amesema wameona ni fursa nzuri kuja kujifunza
Tanzania kwa sababu wao hawaitumii njia hiyo ya vikundi vya kijamii ila tayari
TARURA wamefanikiwa katika utekelezaji wa miradi yao kwenye wilaya.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi
Victor Seff amesema kwamba matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara kama
mawe yaliyopo kwenye eneo la kazi
inapunguza gharama za ujenzi wa madaraja na barabara kwa zaidi ya asilimia 40.
Kwa upande kwa ushirikishwaji wa
vikundi vya kijamii kwenye ujenzi na matengezo ya barabara Mhandisi Seff
amesema kupitia mradi wa uboreshaji wa
barabara za vijijini ambao ni mkopo rahisi toka Benki ya dunia ambao wanasaidia
kuanzisha, kufundisha na kuviwezesha vikundi hivyo kufanya kazi za matengenezo
ya barabara kwa weledi na umakini.
“Faida kubwa ya kuvitumia vikundi
hivyo inapunguza gharama kwani vinatoka maeneo yale yale zinapopita barabara
pia inasaidia kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani kwani
wanatambua barabara ni mali yao.”
Hata hivyo Mhandisi Seff aliongeza
kusema kuwa wao kama TARURA wapo tayari kushirikiana na Sierra Leone kwa
kuwapatia wataalam wa kufundisha pale panapohitajika.
Timu ya Viongozi na wataalam kutoka
Sierra Leone wapo nchini kwa ajili ya kujifunza ujenzi na matengenezo ya
barabara za wilaya katika maeneo ya mipango, ushirikishwaji wa wananchi pamoja
na teknolojia mbadala na wanatarajia kuvitembelea baadhi ya vikundi vya kijamii
Mkoani Njombe.
0 Maoni