MHANDISI Assa Mwakilembe kutoka Tume
ya Madini Sehemu ya Maabara, amewahimiza wadau katika Sekta ya Madini
kuhakikisha wanatumia maabara ya Tume ili kuwa na uhakika kwenye kazi yao ya
uchimbaji.
Amesema kuwa, maabara hiyo ni eneo
litakaloweza kuwasaidia na kujua wingi na ubora wa madini waliyozalisha au
wanayotarajia kuzalisha ambapo pia itasaidia kupata thamani halisi wakati wa
mauzo.
Mhandisi Mwakilembe ameyasema hayo leo
Oktoba 11, 2024 kwenye Maonesho ya Saba ya
Teknolojia na Uwekezaji kwenye
Sekta ya Madini yanayofanyika mkoani Geita katika viwanja vya Bombambili ambapo
Tume ya Madini inashiriki kwa lengo la
kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika Sekta ya
Madini na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Tume ya Madini inayo maabara ya
kisasa pale Msasani jijini Dar es salaam ambayo inahusika na uchunguzi na
upimaji wa ubora wa sampuli za madini kama mikuo ya dhahabu (bullion),
makinikia ya shaba (copper concentrate), Madini ya kinywe (graphite) kwa kutumia teknolojia adimu na bora ya
kuchoma sampuli katika moto (fire assay method),”amesema Mwakilembe.
Aidha, amesema kuwa jukumu la Maabara
ya Tume ya Madini ni kuhakikisha wadau
wanajua ubora na wingi wa madini wanayozalisha na kuuza, hivyo, maabara ipo
katika maonesho haya kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha wadau wanapata huduma bora ya upimaji sampuli pia kutoa
ushauri wa kitaalam.
Amesema kuwa, mbali na maabara hiyo pia majukumu mengine ya
Tume ni Kuratibu uendelezaji wa Sekta ya Madini kwa Kutoa leseni za Utafiti na
uchimbaji wa madini, kuratibu fursa zitokanazo na uwepo wa Sekta ya Madini na
kuhamasisha ushiriki wa Watanzania kwenye mnyororo wa Sekta ya Madini.
“Aidha, Tume ina jukumu la kusimamia
na kuhakikisha mazingira yanalindwa na wachimbaji. Pia usalama wa maeneo ya
kazi na wafanyakazi wa migodini ikiwa ni pamoja na udhibiti wa uzalishaji wa
taka sumu, uhifadhi wake na mipangilio ya taka hizo kwa kufuata viwango
“standards” vinavyokubalika,” amesisitiza Mhandisi Mwakilembe.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hexad,
ambayo inajihusisha na uchimbaji na utafiti wa madini iliyopo Mgasa mkoani
Geita, Fortunatus Luhemeja amesema kwa sasa wachimbaji wadogo wamekuwa na
mwamko wa kutumia teknolojia ya kisasa na kuishauri Tume ya Madini kufunga
Maabara - Kanda ya Ziwa ili iwe rahisi kutoa huduma kwa urahisi na haraka kwa
wachimbaji.
Amesema kuwa, majibu ya sampuli
yanapaswa kutolewa kwa haraka, mchimbaji anayetaka kujua uchimbaji unakwendaje
ni lazima apeleke sampuli na kupata majibu siku hiyo hiyo badala ya baada ya
siku tatu au nne.
“Kazi zetu kila siku lazima tufanye na
Tume ya Madini, hivyo ikija huku itaturahisishia sana hasa teknolojia ya kuchoma sampuli katika moto (fire assay
method), huku hakuna hiyo tunatumia ‘Acid digestion method’ hivyo ‘fire assay
method’ ikija wachimbaji wengi watakimbilia na itapata soko,”amesema.
Wakati huo huo Luhemeja amesema kwenye
uchimbaji ni lazima wafuate taratibu, kanuni na sheria ambazo Tume ya Madini
imewaelekeza kufanya.
“Hatuwezi kusema tunafanya vizuri kama
Tume ya Madini haifanyi vizuri, tunavyofanya vizuri kwenye uchimbaji wetu wa
madini ya dhahabu ni kwamba kuna usimamizi mzuri sana wa Tume ya Madini na kuna
miongozo inayotolewa ya mara kwa mara,”amesema Luhemeja na kuongeza,
“Utatuzi wa haraka wa migogoro
unaofanywa na Tume ni jambo la kufurahisha, ni kama Tume imejiapiza kutokuwa na
migogoro kwenye Sekta ya Madini hasa kwenye uchimbaji, kuhakikisha Sekta inakua
kwa kasi bila vikwazo, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa mfano hapa Geita
imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na sisi wachimbaji kuhakikisha tunafanya
kazi katika mazingira mazuri na kutatua migogoro kwa haki.
0 Maoni