Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inashiriki
maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo (SITE)
yaliyozinduliwa Leo Oktoba 11, 2024 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Ukumbi wa mikutano wa
Kimataifa wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Maonesho haya ya kimataifa ya SITE
yenye kauli mbiu "Tembelea Tanzania kwa uwekezaji endelevu na utalii
usiomithirika" inawakutanisha waoneshaji wa bidhaa na huduma za utalii
takribani 120 kutoka ndani na nje ya nchi.
Ujumbe wa TAWA umeongozwa na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mej. Gen (Mstaafu) Hamis Semfuko akiambatana
na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa
maonesho haya, Meja.Jen (Mstaafu) Semfuko amesema TAWA inatumia maonesho ya
SITE kunadi mazao yake ya utalii ikiwemo utalii wa malikale unaofanyika katika Hifadhi
ya Urithi wa utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani pamoja na Kunduchi.
Sambamba na hilo, TAWA inatumia maonesho haya ya kimataifa
kutangaza bidhaa zake za Utalii wa picha
zinazopatikana katika Mapori ya Akiba ya Pande (Dar es Salaam),
Wamimbiki (Pwani), Mpanga/Kipengere (Njombe na Mbeya), Kijereshi (Simiyu)
sanjari na Utalii wa Uwindaji unaofanyika katika maeneo mengi yaliyo chini ya
Usimamizi wa taasisi hii nchini.
Maonesho ya SITE, yanatarajiwa
kufanyika kwa muda wa siku tatu na yatafikiwa kikomo Oktoba 13, 2024.
Na. Joyce Ndunguru- Dar es Salaam
0 Maoni