Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Taasisi za Elimu, sekta binafsi na wadau wa sekta ya elimu nchini kuhakikisha
walimu wanajengewa mazingira bora ya kazi ili watimize majukumu yao kwa
ufanisi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati
akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu iliyofanyika leo Oktoba
11,2024 Bukombe mkoani Geita,
Aidha, amewataka kuimarisha programu
za mafunzo kwa walimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia huku
akiwataka waajiri kuwapa mafunzo walimu pamoja
na Taasisi zinazohusika na udhibiti wa ubora waendelee kutimiza majukumu
yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali katika
kuboresha sekta ya elimu nchini imeendelea kuboresha na kusimamia miundo ya
watumishi wakiwemo walimu“ Serikali imeboresha stahiki za msingi za watumishi
kwa kupandisha madaraja na kuhakikisha wanapata nyongeza ya mishahara yao kwa wakati,”
Ametaja maboresho mengine “ Serikali
imeimarisha miundombinu mahali pa kufanyia kazi ikiwemo kuhakikisha kuna
madarasa, mabweni na sasa tumeingia kwenye ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na
kuimarisha ajira zao.”
Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa
katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni
229.9 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya walimu huku akiwataka
Maafisa Utumishi kuwasilisha orodha ya walimu wengine wanaohitaji kulipwa nao
ili Serikali iweze kuwalipa.
“ Walimu 601,668 nchi nzima
wamepandishwa madaraja na Serikali imetumia shilingi trilioni 1.3 kuwalipa. Na
niwatake Maafisa Elimu kuwatembelea walimu vijijini na kusikiliza kero zao,”
amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, imeelezwa kuwa Serikali itaendelea
kufanya kazi na Chama Cha Walimu Tanzania ili kujadili masuala ya sekta ya
elimu na kuwa Serikali inatambua mchango wao huku ikiwataka walimu kujiendeleza
katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya kutumia
mtandao kujielimisha.
Akizungumzia tukio la Siku ya Mwalimu
Bukombe, Waziri Mkuu amesema tukio hilo linatoa tathimini ya masuala ya elimu
wilayani humo na kumpongeza Dkt. Biteko kwa kudhamini na kuendeleza siku hiyo
kwa kuwa inaongeza jitihada za viwango vya ufaulu.
Waziri Mkuu amesema katika kuboresha
sekta ya elimu na michezo nchini Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan inajenga shule 10 za michezo na imeiongezea bajeti Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zaidi
ya shilingi bilioni 200 ili kukuza na kuboresha sekta ya michezo nchini.
Pia, Waziri Mkuu ameitaka Mifuko ya
Hifadhi za Jamii kuhakikisha walimu wanapata taarifa za michango yao kwa wakati
pamoja na pensheni zao wakati wa kustaafu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia
amezindua zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura na kutoa
wito kwa Watanzania kujitokeza na kujiandikisha katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewashukuru walimu wa Tanzania kwa
kuendelea kuheshimisha taaluma yao na
kuwa chanzo cha maarifa kwao hakitoki kwingine isipokuwa kwao hivyo wailinde
kwa wivu mkubwa taaluma hiyo.
Dkt. Biteko amebainishwa sababu ya
Wilaya ya Bukombe kuadhimisha Siku ya Mwalimu ni kuwa mwaka 2015 wakati
anachaguliwa kuwa Mbunge, wilaya yake ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika
mitihani ya Taifa.
“Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo
mabaya na wao wakaniambia tusiwaache
nyuma hivyo tulianza kukutana na kufanya tathimini na sasa tunafanya
vizuri,” ameeleza Dkt. Biteko.
Ametaja kuongezeka kwa viwango vya
ufaulu kila mwaka “Katika matokeo ya mwaka jana darasa la saba mkoa tulikuwa
nafasi ya pili, darasa la nne tulipata wastani wa asilimia 78 na kuwa nafasi ya
pili kimkoa.
Ameendelea Kidato cha pili tulikuwa na
ufaulu wa asilimia 98 na mitihani ya kijipima ya Wilaya ya Bukombe tumeshika
nafasi ya tatu hivyo niliona tutenge
siku moja ya kusema asante mwalimu.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa walimu
nchini wasivunjike mioyo waendelee kufanya kazi yao na kuwa maisha yao ni
kielelezo cha mafanikio katika Taifa na kuwa wao ni nyota inayoangaza na yeye
ataendelea kushirikiana nao.
“Nataka niwaambie walimu wote nchini
Serikali inathamini na kutambua mchango wenu kwa Taifa letu na Rais Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya
jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha
maslahi yenu na tayari amepandisha walimu 1,036 wamepandishwa vyeo,” amebainisha
Dkt. Biteko.
Katibu wa Chama Cha Walimu, Tanzania
Mkoa wa Geita, Pauline Tinda amesema kuwa tangu mwaka 2019 Wilaya Bukombe
imekuwa ikiadhimisha Siku ya Mwalimu ambayo inalenga kutekeleza maelekezo ya
UNESCO ya kuwatambua na kutoa tuzo za umahiri kwa walimu wa shule za msingi na
sekondari wanaofundisha masoma ya kusoma kuandika na kuhesabu.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa
kuendelea kuboresha utendaji kazi kwa walimu ma ustawi wa walimu kwa kufanya
jitihada mbalimbali ikiwemo kuwapandisha madaraja.
Pia, amemshukuru Dkt. Biteko kwa
kudhamini maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani na kuendelea kuthamini mchango
wao katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB,
Abdulmajid Nsekela amesema kuwa benki huyo inatambua umuhimu wa walimu nchini
na kuwa watu wengi wamefanikiwa kutokana na mchango wao.
“Sisi tunawapongeza walimu wote
nchini. Tumeendelea kuunga jitihada nzuri zinazofanywa ili mwalimu awe na
mazingira mazuri ya kufanya kazi. Hadi sasa tumetoa zaidi ya shilingi
bilioni 1 ili kununua madawati na leo tunachangia
madawati 500 na hii tufafanya ili elimu iwe bora nchini sambamba na kuwa mdau
muhimu kwa walimu ikiwemo kuendelea kusikiliza maoni ya walimu nchini,” amesema
Nsekela.
Mkurugenzi wa Jembe Limited, Bw. Dkt. Sebastian Ndege amemshukuru Dkt.
Biteko kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika Siku hiyo ya Mwalimu kwa kuwa
imekuwa nafasi nzuri kwao kushirikiana na walimu wa Wilaya ya Bukombe.
0 Maoni