Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza kwenye
miundombinu ya vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba katika kuboresha huduma kwenye
hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Ambapo katika kipindi cha miaka
mitatu, Serikali imenunua mashine za altrasound 457 na hivyo kufikisha idadi ya
mashine 970 ambazo zimesambazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali
ya Taifa, Hospitali maalum, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali
za Wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 9,
2024 jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu
wa Chama cha Wana Radiolojia Tanzania
(TARA), lenye kaulimbiu inayosema “Tafasiri ya Majibu ya Vipimo na Maadili
(Pattern Recognition and Ethics)”.
Akifafanua zaidi kuhusu uwekezaji
uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, Dkt. Biteko amesema “
Serikali imeweza kununua mashine za kidigitali za x-ray 386 hivyo kufikia jumla
ya mashine 469, kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa, Hospitali ya Maalum,
Hospitali ya Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya na Vituo
vya Afya.”
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha
huduma katika Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalumu na Hospitali za Kanda na kufikisha jumla ya mashine saba za MRI
zilizonunuliwa na kuwa na mashine za MRI 13 katika hospitali za umma pamoja na
kusambazwa kwa mashine za CT scan katika mikoa yote nchini.
“Kama Mhe. Rais asingefanya uwekezaji
huu mkubwa ni fedha kiasi gani zingeenda
kutumika nje ya nchi, lakini vifaa pekee haviwezi kutoa majibu isipokuwa nyinyi
wataalamu, kwa niaba ya Serikali tunawashukuru sana na tunatambua mchango
wenu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Serikaki si tu inataka
kuimarisha sekta ya miundombinu na maji bali pia kuboresha afya za Watanzania
na kuwa kwa sasa nchi imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya
afya.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka
wanaradiografia kufanya kazi kwa weledi, kuiheshimu taaluma yao, kuilinda na
kuionea wivu kwa kuwa Serikali licha kuwekeza katika vifaa inaona umuhimu wao
na ndio maana imeendelea kuwasomesha
wataalamu hao.
“ Hakuna mtu atakayekupa heshima ya
taaluma yako bila wewe kuiheshimu, furukuteni ili mtu aone umuhimu wenu,
furukuteni hakuna sababu ya kulalamika nendeni mkawahudumie watu kwa upendo ili
kweli waone Serikali yao ipo kwa ajili ya kuwahudumia na ilindeni taaluma yenu
kwa wivu mkubwa,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Vilevile, ameelekeza Taasisi za TMDA,
NHIF, na TBS nazo zipate wa radiografia katika ofisi hizo ili kuleta ufanisi wa
kazi katika maeneo yanayohusu huduma za radiolojia. Sambamba na kuitaka Wizara
ya afya kufanyiakazi changamoto zote wanazokabiliana nazo wanaradiografia
nchini.
Akimalizia hotuba yake, Dkt. Biteko
amewasihi washiriki wa Kongamano hilo kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kwa kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuchagua viongozi
watakaosaidia kuchochea maendeleo katika jamii.
Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin
Mollel amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia amefanya mapinduzi katika sekta ya
afya katika muda mfupi ikiwa ni pamoja kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati
wa uzazi kutoka 400 hadi 100.
“Katika kuboresha huduma za kibingwa
katika taasisi na Hospitali ya taifa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imepata
mashine ya PET-CT ambayo hufanya uchunguza wa awali wa saratani na mgonjwa
kupata matibabu mapema.”
Ameongeza kuwa sasa kuna upatikanaji
wa huduma za kibingwa na mashine za kisasa kwa ajili ya kutibu kwa kutumia
tundu dogo ambazo zinapatikana Taasisi ya mifupa na mishipa ya fahamu (MOI),
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI) na
Hospitali ya Benjamini Mkapa.
Dkt. Mollel amefafanua kuwa watoto
wenye vibiongo wana uwezo wa kunyooshwa mgongo kupitia vifaa vilivyonunuliwa na
Serikali na wagonjwa wa uvimbe wa chini ya sakafu ya ubongo, pia Serikali
imenunua vifaa vinavyoweza kutibu ugonjwa huo bila kufungua ubongo.
“ Tanzania ni nchi ya nne Afrika
kumiliki PET SCAN ya kumgundua mtu mwenye aina yoyote ya kansa na kutibu ndani
ya nchi bila kwenda nje, pia nchi yetu
ina kiwanda cha kuzalisha mionzi tiba na kabla ya hapo ilikuwa
inanunuliwa kwa gharama kubwa nchini Afrika Kusini au Uturuki, hivyo tumepunguza
rufaa za nje ya nchi kwa asilimia 97,” amesema Mhe. Dkt. Mollel.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.
Paul Makonda amesema kuwa katika Mkoa wake Serikali imetoa shilingi bilioni 72 katika sekta ya afya ambapo shilingi bilioni 32 imetumika kwa
ajili ya kununua vifaa tiba na dawa,
aidha fedha nyingine zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali
katika ngazi mbalimbali.
“Ninamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kupitia wewe kwa kazi
kubwa nzuri aliyofanya katika
sekta ya umeme ikiwemo uendelezaji wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na hadi mradi huo kukamilika na
kuanza kutoa umeme ambao unachagiza ukuaji wa uchumi. Arusha tumezindua mradi
wa REA tutaenda kukamilisha kupeleka
umeme katika vitongoji 1025 tunakushuru sana kwa usimamizi wako katika miradi
hii,” amesema Mhe. Makonda.
Rais wa Chama Cha Wanaradiografia
Tanzania (TARA), Bw. Bakari Msongamwanja amesema kuwa TARA iliundwa mwaka 1976 kwa lengo la kuwakutanisha
wataalamu wa radiografia pamoja na kuboresha taaluma hiyo nchini na kimataifa.
Bw. Msongamwanja amebainisha kuwa TARA
imekuwa na uhusiano mzuri na vyama vya kitaaluma Afrika na duniani na hivyo
imeweza kushika nafasi mbalimbali ikiwemo kuongoza dawati la elimu Kanda ya
Afrika.
Ameongeza kuwa TARA imeshiriki katika
kazi mbalimbali za kukuza taaluma ya radiologia nchini ikiwemo kuandaa kanuni
za mpango wa elimu endelevu.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutenga
fungu na kusaidia wanaradiografia kujiendeleza tutajitahidi kuhakikisha
wataalamu wanafanyakazi kwa weledi na kuzingatia maadili,” amesema Bw. Bakari.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni