Polisi kuendelea kutoa elimu ya Haki Jinai kwa JU

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishna wa Polisi (CP), Benedict Wakulyamba, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa Jeshi la Uhifadhi nchini ili liweze kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizoanzisha jeshi hilo.

CP. Wakulyamba ameyasema hayo jana 22, 2024 alipotembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane na kuteta na maafisa na askari kutoka TANAPA, TAWA na TFS ndani ya ukumbi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.

Akiongozana na Warakibu wawili kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dodoma CP. Wakulyamba alisema, "Jeshi la Polisi litashirikiana nanyi  kutoa elimu na mafunzo mbalimbali hususani juu ya kufuata kanuni za Haki Jinai zinazohusisha ukamataji salama, kuheshimu  haki za binadamu na kutii sheria za upekuzi na kuhodhi mali za uhalifu.”

Aidha, amewataka maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi kuendelea  kuimarisha ulinzi na kusimamia Maliasili zilizopo kwani Taifa lina imani kubwa sana kwenu ndo maana mmepewa dhamana hiyo.

Katika ziara hiyo, CP Wakulyamba, licha ya kutoa mafunzo, pia ametembelea na kuteta na askari wa Lamai na Kenyanganga ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti wilaya ya Tarime Mkoani Mara.

  Na. Brigitha Kimario- Mwanza

Chapisha Maoni

0 Maoni