Wananchi wa kata za Ibindi na Itenka
katika Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wameeleza
kufurahishwa na ukamilikaji wa Daraja la mawe la Ibindi lenye urefu wa mita 16
katika barabara ya Ibindi-Itenka 'A' lililojengwa na Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA).
Wakieleza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha mradi huo ambao umeunganisha Kata za Ibindi na Itenka na kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibindi, Bw.
Lukwai Dotto, ameishukuru serikali kwa kujenga daraja hilo ambapo kwasasa
wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati na uzalishaji wa mazao unaendelea ambapo
wameahidi kuilinda miundombinu ya daraja hilo kwa nguvu zote ili liweze kudumu
kwa muda mrefu.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa mradi huu
maana ilikua vigumu kwa wananchi kuvuka upande wa pili hasa kipindi cha masika,
pia ilikua vigumu hata kwa wanafunzi kupita eneo hili lakini kwa sasa
panapitika kwa urahisi na wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati,” alisema.
Naye, Yusuph Shagungu mkazi wa kijiji
cha Ibindi, ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limeweza
kusaidia shughuli za usafiri na usafirishaji na wananchi wanazifikia huduma za
kijamii kwa urahisi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa
TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi alisema, daraja hilo limejengwa
kwa gharama ya shilingi milioni 286 kwa kutumia teknolojia ya mawe ambayo ni
nafuu pia imerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa
maeneo hayo ambao wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini na
kilimo.
“Daraja hili ni kiungo muhimu kuelekea
Manispaa ya Mpanda, pia wawekezaji wamefika eneo hili, kuna viwanda vya wachina
ambavyo vimesaidia kukuza uchumi wa wananchi, pia utekelezaji huu umewezesha
wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi,” alisema.
0 Maoni