Wananchi katika Wilaya za Mbogwe na
Bukombe mkoani Geita wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza
miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi na kuchochea upatikanaji wa
maendeleo kwa kasi.
Hayo yamebainika jana Oktoba 8, 2024
katika muendelezo wa ziara ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo wilayani Mbogwe na Bukombe
inayofanywa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde mkoani Geita kwa niaba ya
Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan.
Dkt. Zakayo Sungura akisoma taarifa ya
mradi wa ujenzi wa hospitali Wilaya ya Mbogwe, amesema kuwa , kuanzia mwaka wa
2019/2020 mpaka kufikia mwaka wa 2024/2025 zaidi ya bilioni 2.7 zimepelekwa kwa
ajili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali katika kata ya Mbogwe.
Dkt.Sungura ameishukuru serikali kwa
kukamilisha ujenzi wa hospitali ya
wilaya pamoja kupokea vifaa tiba vitakavyo saidi wananchi wa Mbogwe na maeneo
ya karibu kwa kuwa awali iliwalazimu kwenda Wilaya ya kahama kupata huduma
hizo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkuu
wa Wilaya ya Bukombe Mhandisi Paskasi Muragili amesema kuwa kwa kipindi cha
miaka 3 Wilaya ya Bukombe imepokea fedha za miradi ya maendeleo takribani Tsh
45 bilioni ambazo zimewekezwa kwenye sekta ya
Afya, Barabara , Nishati ya umeme
na sekta ya elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Martin
Shigella amemshukuru Mh. Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi ya
maendeleo kufikia zaidi ya Tsh 800 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu na
kusema kwamba miradi hiyo imesaidia kuchochea ukuaji wa kasi wa Mkoa wa Geita.
Akizungumza na Wananchi wa Wilaya za
Bukombe na Mbogwe Waziri Mavunde amesema
kuwa Mkoa wa Geita ni kati ya mikoa iliyopokea fedha nyingi za miradi ya
maendeleo kwenye nyanja ya Afya, Elimu, Miundombinu, Nishati na uwezeshwaji
wananchi kiuchumi.
“Mh. Rais Samia amefanya kazi kubwa
sana mkoani hapa,nimeona idadi ya shule mpya nyingi zimejengwa,nimeziona
Hospitali za Wilaya,Vituo vya Afya na Zahanati kila kona,nimeona barabara mpya
za lami,miradi ya maji na utekelezaji wa kupeleka umeme vijijini,” amesema Mh.
Mavunde na kuongeza,
“Ni dhahiri kwamba wanaGeita
mtakubaliana na mimi kiasi cha Tsh 800 bilioni kilicholetwa mkoani hapa
tunauona utekelezaji wa kweli wa miradi ya maendeleo.”
Waziri Mavunde pia aliupongeza mkoa wa
Geita kwa kuwa kinara katika kuchangia kwenye sekta ya madini ambapo kwa mwaka
wa 2024/2025 imepanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 246.
Waziri Mavunde yupo mkoani Geita kwa
ziara ya kikazi ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo mkoani Geita.
0 Maoni