Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe amewahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika vituo vya kujiandikisha
wapiga kura ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa
kufanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba
11, 2024 mara baada ya kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura katika Kituo
cha Kujiandikisha Mpiga Kura cha Shule ya Msingi Bulangwa kilichopo Wilaya ya
Bukombe, Mkoa wa Geita.
“Ninawashukuru sana kwa kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha ni jambo la muda mfupi ni imaani yangu kuwa mtamaliza kwa
wakati ili muweze kwenda kuendelea na shughuli zenu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Zoezi hili linaanza leo
hadi Oktoba 20, 2024. Wananchi wa Bulangwa mjitokeze waandikishaji wamejiandaa
vizuri na tunataka tuone orodha ya watu wote ili muda ukifika muweze kupiga
kura,” amesema Dkt. Biteko.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.
Martine Shigella amempongeza Dkt. Biteko kwa kushiriki zoezi hilo la
kujiandikisha na kusema kuwa ameonesha mfano kwa wananchi wa Bukombe na
kuwataka wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ili washiriki katika uchaguzi wa
kidemokrasia.
“Tuendelee kuwasihi wananchi kutoka
kila kitongoji kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura kwa kuwa yametengwa
maeneo ya kutosha ili kuwawezesha wananchi wote wenye sifa muweze kupata fursa
hiyo,” amesema Mhe. Shigella.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Bw. Lutengano Mwalyibwa amesema kuwa
maandalizi ya kibajeti na miundombinu kwa ajili ya wananchi kujiandikisha
yamefanyika na kuwa Jimbo la Bukombe lina vituo 348 na mategemeo ni kuandikisha
wananchi 109,124.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye foleni ya kujiandikisha katika
Daftari la Wapiga Kura katika Kituo cha Kujiandikisha cha Shule ya Msingi
Bulangwa kilichopo Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita Oktoba 11, 2024 ikiwa ni
maandalizi ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.(Picha
na Habari na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu).
0 Maoni