Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskazi Muragili amesema kuwa Wilaya yake imeendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni yake ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia inayolenga kulinda afya na kutunza mazingira miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza leo Oktoba 10, 2024
wilayani Bukombe mara baada ya semina ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi,
Mhe. Muragili amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuwatumikia Watanzania ikiwa
ni pamoja na kuendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Moja ya changamoto zinazoleta athari
ya afya na kusababisha vifo kwa akina mama ni matumizi ya nishati isiyo safi
mfano kuni na mkaa ambavyo vinatoa hewa isiyofaa na akina mama wa Tanzania wamekuwa wakiathirika kwa kuvuta hewa hiyo
lakini pia ukataji miti unaharibu mazingira yetu,” amesema Mhe. Muragili.
Amefafanua kuwa asilimia 78 ya Wilaya
ya Bukombe ni misitu na asilimia 22 ni eneo la kuishi binadamu ambapo kwa sasa misitu imeharibiwa kwa kiasi
ilkikubwa kwa sababu ya ukataji miti
ikiwemo Msitu wa Taifa wa Kigosi.
“ Vyanzo vya maji navyo vinekuwa vikiharibika
na ndio maana Rais Mhe. Dkt. Samia amekuja na mpango huu wa kugawa gesi kama
leo tunavyogawa mitungi hii ya gesi
kwenu na mkaitumie. Aidha, tuna vijiji 64 ambavyo vyote vina umeme na mwaka wa
fedha 2024/25 vitongoji 62 vitapata umeme na hivyo mtaweza pia kutumia majiko
ya umeme ili kufikia malengo ya Serikali ya asilimia 80 ya Watanzania watumie
nishati safi ya kupikia ikifapo 2034,” amesema Mhe. Muragili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Teknolojia za Nishati Jadidifu na
Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage
amesema kuwa REA imepewa jukumu la
kuhakikisha bidhaa za nishati safi za kupikia zinafika katika kila pembe ya
nchi ili kumuwezesha kila mwananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi
na salama.
"Serikali kupitia REA imetoa
ruzuku kwa bidhaa zote za nishati safi za kupikia lengo ikiwa ni kuhakikisha
hakuna mwananchi anaachwa nyuma na Serikali imeingia makubaliano na watoa
huduma ya kusambaza mitungi na katika kila wilaya ambapo kwa awamu hii kiasi cha
mitungi 3,255 itatolewa kwa bei ya ruzuku katika kila Wilaya,” amesema Mhandisi
Mwijage.
Aidha, Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa
katika Wilaya ya Bukombe, mtoa huduma atakayesambaza mitungi ni Kampuni ya
Manjis ambapo mitungi hiyo ya kilo sita ikiwa kamili na vichomeo vyake
itatolewa kwa shilingi 17,500 tu ambayo ni nusu bei.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
Bukombe, Mhe. Yusuph Yusuph amesema kuwa uwepo wa semina hiyo ya matumizi ya
nishati safi ni muhimu kwa kuwa inalenga kuunga mkono jitihada za Rais Mhe.
Dkt. Samia Suluhu za kuwahamasisha wananchi wa Bukombe kutumia nishati safi ili
kuepuka madhara yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.
Awali wananchi kutoka kata 17 za
Wilaya ya Bukombe wamehudhuria semina ya matumizi ya nishati safi ya kupikia
iliyolenga kuhamasisha wananchi juu ya matumizi yake na kuepusha athari
zinazotikana na matumizi ya nishati isiyo safi.
Sambamba na semina hiyo ambapo
wananchi hao walipata fursa ya kuuliza maswali kuhusu namna ya kutumia mitungi
ya gesi, pia walipewa elimu kuhusu manufaa ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kunufaika na fursa za mfuko huo kwa jamii.
0 Maoni