Vikundi vya Kijamii vinavyofanya kazi
za ujenzi na matengenezo madogo madogo ya miundombinu ya barabara wilayani
Ludewa wameishukuru Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa
kuwapatia kazi ambazo zimeweza kuwainua kiuchumi.
Wakiongea wakati wa ziara ya Ujumbe
kutoka Jamhuri ya Siera Leone waliofika Kata ya Lugarawa na kutembelea vikundi
vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara katika kata hiyo
wanakikundi hao wamesema tangu waingie mikataba na Tarura wamenufaika katika
nyanja mbalimbali ikiwemo ukuaji kiuchumi.
Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Tujipime’
ambacho kina wanachama 22 wanaoishi na VVU Bw. Manyanya Mkinga amesema tangu
kikundi chao kuliposajiliwa mwaka 2019 wamefanikiwa kupata manufaa mbalimbali
kupitia zabuni za TARURA wanazopata.
“Tuliona tukiungana hatuwezi
kunyanyapaliwa wala kujinyanyapaa wenyewe hivyo kwa kazi hizi tunazopata za
TARURA kwakweli tumeweza kuboresha maisha yetu, licha ya kuishi na VVU
tumefanikiwa kufanya kazi kwa ukamilfu, tunawashukuru sana TARURA kwa kutuwezesha
kupata kazi." Amesema Mkinga.
Ametaja manufaa waliyoyapata tangu
walipoanza kufanya kazi za TARURA mwaka 2020 ni pamoja na ujenzi wa nyumba za
kuishi, ununuzi wa mashamba (parachichi na nyuki), kusomesha watoto pamoja na
kujiunga na Bima ya Afya ya (NHIF).
Bw. Mkinga amesema kwa sasa
wanaendelea na kazi ya ujenzi wa daraja mfuto (Vented Drift), kufyeka barabara
Km.5, kujenga mitaro mita 5 na kinga maji kwenye mitaro katika barabara ya
Mundindi-Ngogoma waliyoanza kujenga Septemba na wanatarajia kuikamilisha mwezi
Oktoba mwaka huu.
Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Twili
Lupangala Road Works Bw. Gutfred Mbilinyi amesema kwamba walianzisha kikundi
hicho baada ya kuhamasishwa wa TARURA na
wameweza kunufaika binafsi na wameweza kuanzisha miradi ya kikundi ikiwemo
mashamba, ufugaji pamoja na ununuzi wa bodaboda tatu ambapo Malengo yao ya
baadae ni kununua gari la kubeba mizigo.
Kwa upande Kiongozi wa Ujumbe huo
ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Matengenezo ya Barabara wa nchi hiyo
Bw. Mohamed Kallon amesema wamefurahi kuvitembelea vikundi hivyo na kujionea
kazi wanazofanya vikundi hivyo ambapo mapato wanayoyapata yameweza kuwanufaisha
kwa kujenga nyumba, kununua bodaboda na kusomesha watoto wao na kwa kikundi cha
wanaoishi na VVU amefanya jambo zuri ambalo inawasaidia kupata riziki zao.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Mtendaji
Mkuu wa TARURA ambaye ni Mkurugenzi wa Barabara Mhandisi Venant Komba amesema
ujio wa ugeni huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa pande zote mbili.
Amesema Siera Leone wamevutiwa na
hatua ya Tanzania kuwa na Taasisi ya kitaaluma inayosimamia shughuli za
Barabara za wilaya, mfumo maalumu wa utunzaji wa taarifa za barabara,
teknolojia ya mawe, ushirikishwaji wa wananchi wanapofanya usanifu pamoja na
namna vikundi vya kijamii vinavyosaidia ujenzi na matengenezo ya miundombinu.
0 Maoni