Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka viongozi wa CCM kutenda haki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Novemba mwaka huu.
Akizungumza na viongozi na wanachama
mbalimbali wa CCM Wilaya ya Kahama leo, tarehe 10 Oktoba 2024, ikiwa ni
mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Shinyanga, akiambatana
na Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Amos Gabriel Makalla, na
Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Hamid Abdalla.
Balozi Nchimbi amesema kila mwanachama
wa CCM ana haki sawa na mwingine, akisisitiza kuwa ni kinyume cha maadili ya
CCM kumnyima mtu mwenye sifa bora nafasi ya uongozi kutokana na chuki binafsi.
“Tunakoelekea kwenye chaguzi zetu,
utekelezaji wa haki unatakiwa. Acheni kupanga safu. Viongozi bora ndio
wapitishwe. Ni kosa kubwa la kimaadili ndani ya CCM kiongozi kumkamia
mwanachama… kwamba eti safari hii nitahakikisha fulani anakatwa kwenye chama
chetu. Hiyo hapana, kwani kila mwanachama ndani ya CCM ana haki sawa na
mwingine.”
“Tuna watu, ukimalizika tu uchaguzi
ndani ya Chama chetu, anaanza upelelezi nani ambae hajamuunga mkono na kuanza
kumshughulikia. Hiyo ni tabia mbaya na haikubaliki. Kwani mtu kukupigia kura ni
haki yake, akikunyima kura ni haki yake pia. Kuna wengine viongozi wamejigeuza
kuwa miungu watu. Hiyo hapana. Viongozi wazuri husambaza upendo,” amesema
Balozi Nchimbi.
Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi, na
Mafunzo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Amos Makalla, ametoa wito kwa
Watanzania na wanachama wa CCM kujiandikisha katika daftari la makazi ili
kuhakikisha wanapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Katika hotuba yake, Makalla
alisisitiza kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kila mwananchi anayependa kushiriki
katika kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ya haraka katika maeneo yao.
Aidha, Makalla aliwataka mabalozi wa CCM kote nchini kushirikiana na wananchi kwa kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, akieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha kuchagua viongozi bora kutoka ndani ya chama.
Aliongeza kuwa ni jukumu la mabalozi
kuhakikisha wanachama wa chama tawala wanashiriki kikamilifu ili kuhakikisha
utekelezaji wa sera za chama kwa mafanikio makubwa.
Katibu huyo pia alieleza kuwa ili
maendeleo yafikiwe kwa haraka, ni muhimu kuchagua viongozi wenye weledi na
maono ya maendeleo, akiongeza kuwa chama kinaendelea kutoa mafunzo kwa viongozi
wake ili kuwaandaa vyema kwa majukumu hayo.
Alisema kuwa kuchagua viongozi sahihi
ni hatua ya msingi katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya
Siasa na Mambo ya Nje wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Rabia Abdalla, alisisitiza
umuhimu wa mshikamano na upendo miongoni mwa viongozi na wanachama wa CCM.
Alieleza kuwa kuwa na uhusiano mzuri
kati ya viongozi kunaimarisha utekelezaji wa majukumu yao na kuleta matokeo
bora kwa wananchi.
Rabia aliongeza kuwa viongozi
wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kuonyesha upendo, umoja, na
mshikamano, akisema kuwa hayo ni maadili muhimu kwa kiongozi yeyote anayejali
maslahi ya wananchi.
Alisisitiza kuwa chama kitatilia mkazo
maadili hayo katika kuhakikisha kuwa viongozi wake wanatimiza wajibu wao kwa
ufanisi.
Katika hitimisho, viongozi wote
walikubaliana kuwa ni jukumu la kila mwanachama wa CCM kuhamasisha ushiriki wa
wananchi katika uchaguzi huo kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.
0 Maoni