Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji
na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na
mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo
yameelezwa leo Septemba 20, 2024 Zanzibar na Dkt. Biteko wakati akimwakilisha
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji,
Tathmini na Kujifunza.
Amesema
wataalam wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo na
kuwashawishi kwa hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na
taaluma hiyo badala ya kujisikia wanyonge kitaaluma.
Aidha, Dkt.
Biteko amewataka washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na
baadaye kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa na watu wake. “Inawezekana
katika maeneo yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali
ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe.
Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika
shirika.” Amesema Dkt. Biteko.
Aidha,
amewataka wataalamu hao kusema ukweli na kusimamia taaluma yao. “ Nataka
niwaombe mkajiamini Rais Samia ameahiza na kuelekeza uwepo wa vitengo vya
tathmini ndani ya Serikali, Ofisi ya
Rais, Mipango na Uwekezaji wafanyekazi na kitengo cha ufuatiliaji kilichopo
Ofisi ya Waziri Mkuu mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo
yake kwenye kubadilisha hali za maisha ya watu,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kupitia
kikao hicho, ametoa maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na
kujifunza.
“Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ikamilishe mapema Mfumo Ufuatiliaji na
Tathmini na kuwezesha taarifa za utendaji wa Serikali kupatikana kwa
urahisi.Tume zetu za Mipango zikamilishe uchambuzi wa miradi yote
inayotekelezwa ndani ya Serikali na kila mwaka kutoa taarifa ya utekelezaji.
Namna hii itawezesha Serikali kuona tija ya miradi inayoidhinishwa na
kutekelezwa hapa nchini,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha
ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini
ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini.
Sambamba na TanEA na ZaMEA kuweka mikakati ya kujiimarisha kiuchumi ili ziweze
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa uanzishwaji wake.
Aidha, Dkt. Biteko aziagiza TanEA na ZaMEA
kuwa Sera pamoja na mikakati yake ziwe zinafanyiwa Tathimini kila baada ya
miaka mitatu baada ya kuandaliwa. Hii itasaidia kujua kila hatua inayofikiwa
kwa utelezaji wake pamoja na utatuzi wa changamoto za utelezaji na maboresho
wakati wa uhuishaji wa Sera.
Kwa upande
wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.
William Lukuvi amesema kuwa Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na
Kujifunza lenye kauli mbiu isemayo
‘Kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika
ufuatiliaji na tathmini na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya
maamuzi’ limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.
Ametaja
lengo la Kongamano hilo kuwa ni kuweka
msisitizo kwenye lengo kuu la Serikali la kutoa huduma bora na kwa
wakati kwa wananchi na kuwa katika kutimiza azma hiyo, washiriki wamehamasishwa
kutumia vizuri taaluma na mafunzo mbalimbali wanayoyapata kuhakikisha wanakuwa
jicho la Serikali katika mipango yake, utendaji wake na utekelezaji wa miradi
ili iweze kupata maendeleo.
Aidha, Mhe.
Lukuvi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali
kwa ujumla wake, utekelezaji wa miradi yote nchini na utoaji wa huduma bora kwa
wakati kwa wananchi wote.
Amesema kuwa
marais hao wanafanya hayo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) ya mwaka 2020 ambapo kwa sekta zote umewekwa mkazo wa ufuatiliaji na
tathmini katika utendaji, utekelezaji wa miradi na utoaji huduma.
“Katika
kuimarisha Sekta ya Fedha, ibara ya 20 (f) ya Ilani ya CCM inaitaka Serikali
kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa
ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa ipasavyo na Sekta ya Ujenzi, ibara ya
51(a)(ii) ya Ilani inaitaka Serikali
kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za barabara kwa
kuhakikisha thamani ya ubora wa kazi inaendana na fedha zilizotumika,” amesema
Mhe. Lukuvi.
Naye, Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa
kupitia Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa
wataalamu. Sambamba na washiriki kujifunza mbinu mpya za kuboresha mifumo ya
Ufuatiliaji na Tathmini, hasa kwa kutumia teknolojia na takwimu sahihi ili
kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.
“Kongamano
hili limesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa
Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha
Serikali na wahisani wanatoa huduma zenye tija. Pia, ushirikishwaji wa
waananchi utasaidia kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inawafaidisha moja kwa
moja,” amesema Dkt. Yonazi.
Vilevile
ameongeza kuwa, kongamano hilo limelenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika
utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali
wakiwemo watendaji wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, na
wananchi, aidha, limetoa jukwaa la kujadili jinsi ufuatiliaji na tathimini
unavyoweza kutumika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na
uwajibika.
Kaimu Katibu
Mtendaji Tume ya Mipango, Dkt. Ameir Haji Sheha amesema kuwa ushiriki wa
Kongamano hili limeibuwa haja na mahitaji mbalimbali na kuwa Kongamano hilo limejumuisha washiriki
738 na ameishukuru Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano
wakati wote wa maandalizi wa Kongamano hilo.
0 Maoni