Mkazi wa
Lindi, Bw. Karume Karume (41) aliyesumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za
mwili wake kwa zaidi ya miaka 25, leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya
kufanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili na kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari, Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Rekebishi na Mkuu wa Kitengo
cha Upasuaji Rekebishi Dkt. Laurean Rwanyuma aliyeongoza jopo la watalaam
wenzake kumfanyia upasuaji uliodumu kwa saa nne, amesema baada ya uchunguzi wa
kina kukamilika, iligundulika kuwa Bw. Karume ana uvimbe sehemu mbalimbali za
mwili wake hasa shingoni, begani na kifuani na ugonjwa huo unaitwa Plexiform
Neurofibromatosis ambao matibabu yake ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji ambapo
Agosti 30 mwaka huu alifanyiwa upasuaji.
Dkt.
Rwanyuma amesema, ugonjwa aliopata Bw. Karume siyo wa kuambukiza bali ni
ugonjwa wa kuzaliwa nao ambao ameurithi kutoka kwa ama mmoja wa wazazi wake au
wazazi wake wawili wenye ugonjwa huo ambao hushambulia mishipa ya fahamu na
kujitokeza kwa njia mbalimbali.
Naye,
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, amesema mara baada ya kumpokea Bw.
Karume Agosti mwaka huu, hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha Bw.
Kalume anaonwa na madaktari bingwa na kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini
mwenendo wa matibabu yake na kuwapongeza waandishi wa habari kumuibua mgonjwa
huyo na kumleta hospitalini hapo kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa
upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano
unaompa faraja na tabasamu.
Dkt.
Mhaville amewaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa
watu wasiokuwa na uwezo akiwemo Bw. Karume ili kukamilisha malipo ya huduma
alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Kwa upande wake, mjomba wa Karume Salum Ahamad Idobelele amesema alianza kuangaika na Karume akiwa na miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo na baadae kubahatika mwaka huu kukutana na waandishi wa habari kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufaa ya kuja Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mkurugenzi
wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali hiyo, katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini
Dar es Salaam.
0 Maoni