Tamasha maarufu la Mt Hanang’ Nyama Choma Festival 2024
limefana kwa mara nyingine, likivutia watalii wa ndani zaidi ya 120 katika
Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Hanang’ iliyopo katika mji wa Katesh,
mkoani Manyara.
Tamasha hili, ambalo linafanyika kila mwaka, lilifanyika
msimu huu kuanzia tarehe 31 Agosti hadi 1 Septemba 2024, limewavuta wananchi
kutoka maeneo mbalimbali nchini kutokana na Hifadhi hio kuwa ni kivutio cha
kipekee kwa watalii wa ikolojia na utamaduni.
Mratibu wa Tamasha Hilo na Afisa Utalii wa Mt Hanang’, Elizaberth
Mbunda amesema tamasha hilo lenye lengo la kutangaza vivutio vya kitalii ndani
ya hifadhi hiyo limekuwa likizidi kupata umaarufu mkubwa kutokana na uwepo wa
maeneo mbalimbali ya kitamaduni, kihistoria na urithi kama vile maeneo
matakatifu ya jamii za Wabarabaig na maziwa ya soda ya Balang'dalalu na
Gendabi.
“Mlima Hanang' ni eneo maarufu kwa mazoezi ya kupanda Mlima
Kilimanjaro lakini pia una mandhari za kuvutia, sasa ili kukuza shughuli za
utalii tumeamua kuja na nyama choma festival ambapo washiriki walipata fursa ya
kutembelea maeneo mbalimbali ya kuvutia kama vile msitu mnene, maporomoko ya
maji, na sehemu za matazamio za "viewpoint" ambapo walishuhudia mawio
na machweo ya jua na kisha kufurahia kwa kula nyama choma zilizoambatana na burudani
mbalimbali za usiku, ikiwemo camping, kuota moto, na muziki,” anasema.
Aidha, amesema kuwa hali ya utalii imeendelea kuwa shwari
licha ya athari zilizowahi kusababishwa na maporomoko ya maji hapo awali.
Kwaniaba ya Mkuu wa Wilaya Ndugu Athumani Likeyekeye katibu
tawala wilaya ya Hanang aliipongeza TFS kwa kuendelea kuboresha utalii katika
Hifadhi ya Mlima Hanang’.
Kamanda wa Kanda ya kati – TFS, Kamishna Msaidizi mwandamizi
Mathew Kiondo ni miongoni mwa viongozi walishiriki tamasha hilo “niwapongeze
waandaaji kwa ubunifu wao na kuendeleza uhamasishaji wa wananchi kuja kujionea
shughuli za utalii ikolojia ndani ya Hifadhi ya Mlima Hanang’.
Hifadhi ya Misitu ya Asili ya Mlima Hanang' ina eneo la
hekta 5,871 katika kimo kinachotofautiana kati ya mita 1860 hadi 3423 juu ya
usawa wa Bahari. Mlima Hanang’ ni mlima wa nne kwa urefu nchini Tanzania baada
ya Kilimanjaro, Meru, na Lolmalasin ukiwa na kimo cha mita 3423 juu ya usawa wa
bahari.
Hifadhi ya Misitu ya Asili ya Mlima Hanang' ina shughuli nyingi za kiikolojia na kiutamaduni kama vile ngoma za jadi, mapambo ya kitamaduni, kutembelea maeneo matakatifu, kuonja pombe za kienyeji, kupanda mlima na kufuatilia njia, kutazama wanyamapori, kutazama ndege, matembezi ya msituni na upigaji picha. Pia, kuna fursa ya kutazama Bonde la Ufa na mapango unavyopanda kuelekea kilele cha Mlima Hanang'.
0 Maoni