Wizara ya Maliasili na Utalii ametoa
wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda maeneo yanayohifadhiwa kisheria pamoja
na kuhakikisha udhibiti wa Wanyamapori hao unafanyika kwa njia mbalimbali
ikiwemo wananchi kuacha kuvamia na kulima mazao yanayopendwa na wanyamapori
hususan Tembo pamoja na kuchunga mifugo maeneo ya wanyama hao.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi
Benedict Wakulyamba alipotembelea Kijiji
cha Butuli kinachopakana na Pori la
Akiba Maswa na kushuhudia namna baadhi ya wananchi wakiendesha shughuli za
kibinadamu pembezoni mwa mpaka na wengine ndani ya eneo lililohifadhiwa
Kisheria.
Akiongea na Maafisa na Askari wa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), CP. Wakulyamba amesema kuwa Mhe. Waziri
Balozi Dkt. Pindi Chana ameagiza jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha
wananchi wanakuwa salama pamoja na mali zao na hasa kudhibiti vifo
vinavyotokana na Tembo.
CP. Wakulyamba ameongeza kuwa Waziri
Balozi Dkt. Chana ameagiza kuendelea kujenga mahusiano mema na wananchi
wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuhakikisha wanapatiwa elimu ya
kutosha, pamoja na kuwashirikisha kikamilifu katika mapambano dhidi ya wanyama
hao.
"Sisi wahifadhi tunayafahamu kitaaluma
maeneo tunayoyalinda kwa kuwa tumesomea na tumeletwa hapa kufanya kazi lakini
Wananchi wanaoyazunguka maeneo ya Hifadhi wao wanayafahamu kwa asili,
wamezaliwa hapo, wanaishi hapo hivyo wanayajua kwa undani mkubwa.
Tukishirikiana nao watatusaidia hata kuwajua wahalifu dhidi ya maliasili
zetu", Alisema CP Wakulyamba.
Aidha, CP. Wakulyamba amewataka askari
hao wa TAWA kuzingatia mafunzo waliyopewa na Maafisa wa Polisi Mrakibu wa
Polisi Joseph Jingu na Mrakibu wa Polisi Ocsar Felician sambamba na Afisa
Mhifadhi Edwin Nyerembe kutoka Wizara ya Maliasilina Utalii juu ya Haki za
Binadamu na Utawala wa Sheria. Mafunzo hayo ni utekelezaji wa Maelekezo ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotokana
na maoni ya Tume ya Jinai.
Mafunzo mengine yanayotolewa na
Maafisa hao ni pamoja na matumizi sahii na salama ya Silaha yakilenga kuboresha
utendaji kazi ndani ya Jeshi hilo la Uhifadhi.
Awali akitoa Taarifa ya utekelezaji wa
shughuli Katika Pori la Akiba Maswa,
Kamishna Msaidi wa Uhifadhi Saidi
Kabanda, ambaye ni Kaimu Kamanda wa
Uhifadhi Kanda ya Ziwa TAWA, amesema moja ya jitihada zilizochukuliwa katika Mkoa wa Simiyu ni pamoja na kujengwa
kwa vituo vinne vya kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu, kukarabari
vituo vingine vinne pamoja na kuongeza askari wa Uhifadhi na wa Vijiji (VGS).
Naye Afisa mtendaji Kijiji cha Butuli Emmanuel Fabian machibya ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua zinazochukuwa za kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Butuli katika mapambano dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu hali inayoleta faraja zaidi kwa wananchi.
Na. Sixmund Begashe - Butuli Simiyu
0 Maoni