CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo
(SACCOS) cha Tume ya Madini kimepata hati inayoridhisha katika ukaguzi wa
Hesabu za Chama zinazoishia Desemba 31, 2023 baada ya kufanyiwa ukaguzi na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya
Ushirika (COASCO) Tanzania Bara.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 18, 2024 na
Mwakilishi wa COASCO Amina Kitua, katika
Mkutano wa nne wa mwaka wa Madini SACCOS
uliofanyika katika ukumbi wa Mkandarasi jijini Dodoma.
Amina amesema, zipo changamoto ndogo
za kitendaji zilizoonekana ambazo zimeainishwa na kushauri kufanyiwa kazi kama
mkakati wa kuimarisha Tume ya Madini SACCOS.
“Mikopo iliyotolewa ilifuata taratibu
zote zinazotakiwa, ndio maana kwenye ukaguzi wetu haujagusa eneo la fedha, ila
kuna upungufu uliosababishwa na uchanga wa chama hivyo tumetoa ushauri ili
kuimarisha chama,”amesema Amina.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini
SACCOS, Endrewcus Masero amesema Tume ina watumishi 900 kati yao watumishi 426 ndio wanachama wa
SACCOS idadi ambayo ni ndogo kwa kuwa
lengo ni watumishi wote kujiunga na SACCOS hiyo.
“Katika kipindi cha Januari hadi
Septemba 2024 wanachama wapya 53 wamejiunga ikiwa ni sawa na asilimia 26 ya
lengo la wanachama wapya 200 tulilokuwa tumejiwekea na hivyo kufikisha idadi ya
wanachma 426,”amesema Masero.
Amesisitiza kuwa bado linaendelea zoezi
la kuhamasisha wanachama wapya kujiunga na SACCOS kuanzia Tume ya Madini Makao
Makuu na Ofisi zote za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Katika hatua nyingine akielezea utendaji
wake, Massero amesema SACCOS ya Tume ya Madini imefanikiwa kutoa mikopo ya
Shilingi milioni 394 kwa anachama 86 sawa na asilimia 20.19 ya wanachama wote.
Na. Vicky Kimaro- Dodoma
0 Maoni