Wakulyamba awatunuku vyeo maafisa na askari viongozi TANAPA

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (Uhifadhi) Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba amefunga mafunzo ya uongozi kwa maafisa na askari wahitimu 236 ikiwa ni maafisa 159 na askari 77 Fort Ikoma Serengeti.

Akiongea katika hafla hiyo jana Kamishna Wakulyamba amewapongeza wahitimu na kuwataka maafisa na askari hao kuwa viongozi wa mfano na kuyaishi yale yote waliyojifunza wakati wakiwa mafunzoni.

“Elimu ni ujuzi unaokusaidia kutatua changamoto unazokutana nazo hivyo elimu mliyopata tuione ikiwasaidia kutatua changamoto mnazokutana nazo huku mkisimamia nidhamu na uadilifu ili jeshi letu la Uhifadhi liwe la mfano," alisema Kamishna Wakulyamba.

“Mkafanye kazi kwa weledi na bidii mkifuata taratibu, kanuni, sheria na miongozo ya jeshi letu huku mkijiepusha na matendo yanayofedhehesha jeshi.  Mkazingatie sheria na haki za binadamu,” alisisitiza Kamishna Wakulyamba.

Aidha, Kamishna Wakulyamba amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kupandishwa vyeo maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi. Pia amemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kumtuma kumwakilisha katika hafla hii.

“Naishukuru wizara na viongozi wangu kunipa fursa ya kukutana na kuongea na maafisa na askari wa Uhifadhi wengi kiasi hiki kwani ni nadra sana kuwapa wengi namna hii kwa wakati mmoja kutoka a an majukumu mazito ya uhifadhi na utalii mnayofanya ,” alisema Kamishna Wakulyamba.

Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa amewapongeza wahitimu na wakufunzi wa mafunzo hayo na kusisitiza nidhamu na uwajibikaji kwa wahitimu hususani wanaporudi katika maeneo yao ya kazi.

“Mafunzo mliyoyapata yamewapa ujuzi wa kujieleza, kutafsiri sera na sheria za uhifadhi wa Wanyamapori na misitu, kuandaa mijadala na kusimamia mikakati mbalimbali ya kazi za uhifadhi na utalii.  Ni imani yangu kuwa mnaondoka hapa mkiwa tofauti na mlivyokuja.”

Aidha, Mwishawa aliongeza kuwa Shirika linatambua kuwa mafunzo mliyopata yataongeza tija katika usimamizi wa rasilimali za nchi tulizopewa dhamana ya kuzitunza na kuzilinda ili ziendelee kuchangia pato la Taifa,” aliongeza Kamishna Mwishawa .

Mafunzo hayo ya uongozi kwa maafisa na askari yamefanyika kwa awamu mbili yakilenga kuwajengea viongozi uwezo wa kusimamia nidhamu na kuimarisha mila na desturi za kijeshi ikiwa ni kwa nadharia na vitendo.

Na. Brigitha Kimario- Serengeti

Chapisha Maoni

0 Maoni