Kisiwa cha Rukuba Chafurahia Huduma Mpya ya Afya baada ya Kituo cha Afya Kupatiwa Umeme Jua

 

Katika kisiwa kidogo cha Rukuba kilichoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoani Mara maisha ya wananchi sasa yanaonekana kuwa na mwangaza mpya.

Hadi hivi karibuni, wakazi wa kisiwa hiki walikuwa wakipambana na adha kubwa ya usafiri kwa boti ili kuwapeleka wagonjwa wao kwa huduma za upasuaji mdogo nje ya kisiwa hicho. Hali hiyo ilikuwa kero kubwa, hasa wanawake walipokuwa wanahitaji upasuaji wa dharura.

Kisiwa cha Rukuba, kilichopandishwa hadhi kuwa kijiji mnamo mwaka 1974, kilikuwa kinategemea huduma ya Zahabati, na wagonjwa walilazimika kusafiri kwa boti kwa muda mrefu ili kufika hospitalini. Safari hii ilikuwa ni ngumu na yenye hatari, hasa kwa wagonjwa waliokuwa na hali mbaya.

Hata hivyo, mabadiliko makubwa yamekuja baada ya serikali kutekeleza mradi wa kujenga Kituo cha Afya chenye umeme jua. Rais Samia Suluhu Hassan, akiungana na mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, walishughulikia ujenzi wa kituo hiki kwa gharama ya shilingi milioni 500 na vifaa tiba vilivyogharimu shilingi milioni 100.

Wakazi wa Rukuba sasa wanaweza kusema kwamba maisha yao yameimarika. Hassan Juma Ibrahim, mmoja wa wakazi wa kisiwa hicho, alieleza furaha yake kwa kusema, "Mbunge wetu amefanya kazi kubwa sana, amefanikisha kutuletea shilingi milioni 345 kwa ajili ya umeme jua wa mradi wa REA. Umeme huu utawezesha wagonjwa kupata huduma za matibabu nyakati za usiku bila shida yoyote."

Abdalah Suma aliongeza kwa kusema, "Awali ilikuwa vigumu sana wakati mama alihitaji upasuaji mdogo wa dharura. Lakini sasa, umeme jua utaondoa matatizo yote hayo. Hii ni neema kwa sekta ya afya na pia kwa elimu, kwani umeme huu utatumika katika taasisi za elimu pia."

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma, Thomas Kipango, alieleza jinsi kituo hicho kilivyokuwa msaada mkubwa kwa jamii. "Tulikuwa tunakabiliwa na ugumu wa kusafirisha wagonjwa kwa boti, ambapo mara nyingine ilikuwa inachukua zaidi ya saa moja na nusu kabla ya kufika matibabu. Sasa, adha hiyo imekwisha," alisema Kipango.

Kisiwa cha Rukuba, ambacho kinategemea uvuvi kama chanzo kikuu cha uchumi, kimepata suluhu ya huduma bora za afya na umeme jua, na hivyo kuifanya jamii yake kuwa na matumaini mapya.

Chapisha Maoni

0 Maoni