Waziri Kijaji akutana na ujumbe wa Kamisheni ya Bonde la Kongo

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameonana na ujumbe kutoka Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, ulioongozwa na Mhe. Arlette Soudan–Nonault, Waziri wa Mazingira wa Jamhuri ya Congo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania, Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo, na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha juhudi za mazingira za kikanda na kukuza suluhu za pamoja kwa mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa utofauti wa kibaiolojia katika Bonde la Congo.

Aidha, Mhe. Kijaji, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, amepokea hati ya makubaliano (MoU) ya Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, ambayo ataiwakilisha kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hatua zaidi.

Kwa upande wake, Mhe. Arlette Soudan–Nonault ameshukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka Tanzania. Ameahidi kwamba timu ya wataalamu wa Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, chini ya Jean Paterne Megne Ekoga, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Utawala wa kamisheni, itarejea hivi karibuni kwa ajili ya kushirikiana katika upembuzi wa miradi ya kipaumbele ambayo itapata fedha na kuanza utekelezaji.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nonault alimuomba Mhe. Kijaji kuhakikisha anashirikiana kwa karibu na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na mwakilishi wa nchi katika Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, Prof. Dos Santos Silayo, ili kuhakikisha serikali na sekta binafsi zinashiriki katika kulinda na kuhifadhi bioanuai na misitu ya bonde la Congo, ambayo ina umuhimu mkubwa katika ustahimilivu wa bonde la Congo na dunia kwa ujumla, na pia katika kunufaika kiuchumi.

Awali, Mhe. Nonault, aliyeambatana na ujumbe wa watu nane, alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.), ambaye alimhakikishia kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na kamisheni hiyo na mfuko wake na iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha nyaraka zinazohitajika ili kufikia lengo la Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo.

Aidha, Waziri huyo wa Congo alifanya kikao na wadau wa Asasi zisizo za Kiserikali/Asasi za Kiraia (NGOs, CBOs, na CSOs) zinazojihusisha na shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, akizitaka kushiriki kikamilifu katika kusukuma mbele agenda ya mazingira nchini kwa kuchangamkia fursa za uwepo wa fedha katika Mfuko wa Bluu wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo.

“Nafahamu kuwa NGOs mmekuwa wadau wakubwa katika kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo. Hatuwezi kupata uchumi endelevu bila kudhibiti mazingira yetu. Uharibifu wa mazingira duniani ni mkubwa, na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa. Kamisheni ina mfuko wenye fedha zitakazowawezesha kutimiza malengo yenu katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu agenda hii muhimu ya mazingira,” anasema Mhe. Nonault.

Ikumbukwe kwamba Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo unajumuisha nchi wanachama 17, ambazo zinapata fursa mbalimbali, ikiwemo kuandika miradi na kuomba ushirikiano ili kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa, hasa katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la watu duniani.

Nchi wanachama wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo ni: Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kati ya Afrika, Chad, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea Ikweta, Ufalme wa Morocco, Gabon, Kenya, Rwanda, Sao Tome na Principe, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia.



Chapisha Maoni

0 Maoni