Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kujipanga na kuweka mikakati ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kufanikisha matarajio ya ya Serikali na wananchi.
Hayo ameyasema leo jijini Arusha wakati akizungumza na
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NHIF waliokutana kuweka mikakati ya
uboreshaji wa huduma kwa wadau wake.
“Jambo la Bima ya Afya ni kubwa, lazima tujipange vizuri
katika utekelezaji wake, Sheria na Kanuni zimeshasainiwa na katika hili
niwahakikishie Serikali iko na ninyi katika kila hatua ili muweze kufanikisha
hili,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Amesema kuwa ili kufanikisha suala hilo, Mfuko ujikite
katika matumizi ya Mifumo na kuongeza ubunifu katika vitita vyake ili kuleta
ufanisi na tija katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake.
Akizungumzia utendaji kazi, amewakata Watumishi kuwajibika
katika maeneo yao kwa kutambua dhamana kubwa iliyowekwa na Serikali kwa Mfuko
kuhudumia wananchi wake.
“NHIF mna dhamana kubwa sana na ni nguzo kubwa katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu nchini, hakikisheni mnaboresha
utendaji kazi wenu ili huduma mnazozitoa ziweze kwenda na wakati au mahitaji ya
sasa,” amesema Katibu Mkuu.
Aidha, ametumia fursa hiyo, kuonya baadhi ya wanaojihusisha
na vitendo vya udanganyifu na kuwataka kuacha mara moja na badala yake kuwa
walinzi wa huduma ili Mfuko uendelee kuwa hai na kutoa huduma bora.
Katibu Mkuu amempongeza Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka kwa
kuaminiwa na kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan kuiongoza NHIF ambayo ni taasisi nyeti na nguzo katika sekta ya
afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Irene Isaka,
amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa watumishi wote wa Mfuko wako tayari kutekeleza
suala la Bima ya Afya kwa wote ili matarajio ya Serikali na wananchi yaweze
kufikiwa.
“Tutafanya kazi kwa nguvu zote na weledi mkubwa, tumejipanga na tunafanya kazi kubwa kuweka mifumo yetu vizuri ili iweze kurahisisha utoaji wa huduma zetu,” alisema Dkt. Isaka.
0 Maoni