Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayesimamia Utalii, Nkoba Mabula,
ametembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani na kuonyesha matumaini makubwa
juu ya uwezo wa hifadhi hiyo kuwa kivutio kikuu cha utalii nchini, akifananisha
na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mabula
alisisitiza kuwa hadithi za bioanuwai na mandhari yake zinathibitisha kuwa,
ikitangazwa vyema, hifadhi hiyo inaweza kuvutia watalii wengi na kuchangia pato
la taifa.
Akizungumza
baada ya kutembelea hifadhi hiyo Septemba 25, 2024, Mabula aliongeza kuwa
hifadhi hiyo inatoa fursa kubwa kwa utalii wa kiikolojia na inapaswa kupewa
kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya sekta ya utalii. “Kutembea katika
Hifadhi ya Amani ni kama kuwa katika bustani ya furaha na amani. Uzuri wa asili
na utulivu wake, pamoja na sauti za ndege adimu, vinachangia sifa yake ya
kipekee,” anasema.
Mabula
alivutiwa kusikia kuwa hifadhi hiyo, iliyoko katika wilaya za Muheza na Korogwe
mkoani Tanga, ni makazi ya maua maarufu ya "African Violet"
(Saintpaulia), ambayo yana umuhimu wa kiikolojia na kiroho, hasa katika
kuhamasisha nguvu ya msamaha.
Alphonce
Nyululu, Mhifadhi wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani, alisema hifadhi hiyo
iliyoanzishwa mwaka 1997 inajulikana kama moja ya maeneo 12 bora duniani kwa utazamaji
wa ndege, na imeorodheshwa na UNESCO kama sehemu ya Hifadhi za Maisha na
Mazingira Duniani.
Someni
Mteleka, Mkuu wa Kitengo cha Utalii, aliongeza kuwa mapato ya hifadhi hiyo
yameongezeka kutokana na upekee wa rasilimali zake na urahisi wa kufikika, huku
maboresho ya miundombinu yaliyofadhiliwa na mradi wa UVIKO-19 yakiwavutia
watalii wengi zaidi.
Kamanda wa
Uhifadhi wa Kanda ya Kaskazini, James Nshare, alishukuru kwa ziara ya Mabula,
akisema imetoa motisha zaidi ya kukuza utalii wa hifadhi hiyo na kuahidi
kuendeleza juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya
utalii vya Tanzania.
0 Maoni