Akizungumza katika hafla hiyo ya
Kijeshi iliyofanyika Septemba 19, 2025, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA
yaliyopo Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen
(Mstaafu) Hamis Semfuko alimpongeza Kamishna Nyanda kwa kuhitimisha safari yake
ya utumishi na kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa kwanza wa TAWA aliyedumu kwa muda
mrefu na kustaafu akiwa kwenye cheo hiko cha juu katika uongozi wa TAWA.
“Kwa namna ya kipekee ningependa
kukupongeza na kukushukuru Kamishna Mstaafu Nyanda kwa utumishi wako katika
tasnia hii ya uhifadhi na hususan ukiwa kama Kamishna wa TAWA,” alisema Mej.
Jen (Mstaafu) Semfuko.
Sambamba na hilo, Semfuko
aliongeza kuwa chini ya uongozi wa Kamishna Mstaafu Nyanda, TAWA imepata
mafanikio mengi yakiwemo kuboresha maslahi ya watumishi, ujenzi wa miundombinu
pamoja na kuongeza mapato ya Serikali, hususan baada ya uanzishwaji wa kuuza
vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya kielektroniki pamoja na Uwekezaji
Mahiri katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.
“Mambo mengi ya kuijenga TAWA
ikiwemo kubadilisha mifumo, kuboresha maslahi ya watumishi na mambo mengine
yamefanywa chini ya uongozi wa Kamishna Nyanda, yeye akisaidiana na viongozi
wengine ndio wameijenga TAWA kuwa hivi ilivyo sasa,” alisema Mej. Jen ( Mstaafu)
Semfuko.
Kadhalika, Semfuko aliongeza kuwa
Kamishna Nyanda, ameleta mabadiliko mengi ikiwemo kuongeza uadilifu na kuifanya
TAWA kuwa imara zaidi.
“Umefanya kazi kubwa sana katika
kujenga stability ndani ya TAWA, umeiacha TAWA ikiwa tulivu, imara na yenye
nguvu zaidi,” alisema Semfuko.
Kwa upande wake, akitoa salamu za
shukrani Kamishna wa Uhifadhi Mstaafu Mabula Misungwi Nyanda aliishukuru Bodi
ya Wakurugenzi ya TAWA kwa kutoa maono na miongozo iliyoweza kuifikisha TAWA
ilipo sasa. Aidha, aliishukuru Menejimenti ya TAWA na watumishi wote kwa
kuitekeleza miongozo hiyo iliyoleta mafanikio mengi katika Taasisi.
“Menejimenti na watumishi wa TAWA
nyie ndio mliofanya mafanikio haya kuwa kweli, uaminifu wenu, weledi, juhudi na
moyo wa uzalendo mlionyesha katika kulinda rasilimali za wanyamapori ni wa
kupongezwa sana,”alisema Kamishna Mstaafu Nyanda.
Awali, akizungumza kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na
Rasilimali watu, Ndugu. Bernard Mercelline alimpongeza Kamishna Mstaafu Nyanda
kwa kumaliza utumishi wake, Aidha, aliongeza kuwa kwa kupitia majukumu
aliyoyatekeleza ameifanya TAWA ijulikane zaidi ya ilivyokuwa.
“Kwa niaba ya Wizara nichukue
nafasi hii kukupongeza kwa kazi njema uliyoufanya na nikushukuru kwa kazi
nzuri,” alisema Mercelline.
Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi
wa TAWA , Mlage Kabange alimshukuru Kamishna Mstaafu Nyanda kwa kuweka misingi imara na alisisitiza kuwa Menejimenti
itaendelea kuyaenzi na kuyasimamia ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na
Taasisi yanafikiwa kwa viwango vya juu.
Hafla ya Kijeshi ya kumuaga
Kamishna wa Uhifadhi Mstaafu Mabula Misungwi Nyanda iliambatana pia na tafrija
fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Cate Hotel uliopo Mkoani Morogoro.
Na. Joyce Ndunguru, Morogoro
0 Maoni