Balozi wa Tanzania katika nchi za
Nordic, Baltic na Ukraine, Mhe. Mobhare Matinyi, tarehe 18 Septemba, 2025,
alikutana na watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson na Christopher
Thunell, katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm, Sweden,
kujadiliana kuhusu uwekezaji wa teknolojia ya kilimo makini cha umwagiliaji
nchini.
Teknolojia hiyo ya kampuni ya
SPOWDI hutumia mashine ndogo ya nishati ya jua yenye mipira ya umwagiliaji
inayosambazwa shambani kutokea kwenye bwawa dogo. Umwagiliaji huu hufanyika kwa
dakika 15 katika eneo la mita za mraba 500 kwa mara moja.
“Ekari moja yenye mita za mraba
4,000 inaweza kumwagilia kwa muda mfupi tu na kuokoa upotezu wa maji, muda na
pia kusaidia mimea kukua kwa ubora unaostahili na hatimaye kutoa mazao mengi
zaidi,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu Johanson na kuongeza kuwa matokeo yake ni
kuongeza kipato na pia kulima kwa zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka kwa gharama
nafuu na bila kutegemea mvua.
Kampuni hii inakusudia kuwekeza
nchini Tanzania baada ya kuvutiwa na mazingira mazuri ya Tanzania, uchapakazi
wa Watanzania na sera nzuri za serikali katika uendelezaji wa sekta ya kilimo
ikiwemo kusaidia upatikanaji rahisi wa mikopo kwa wakulima.
Tayari kampuni hiyo imeifikisha
teknolojia hiyo katika nchi za Sweden, India, Nepal, Bangladesh, Uswizi na kwa
Afrika imeanza uwekezaji nchini Kenya na hivyo Tanzania itakuwa nchi ya pili.
Balozi Matinyi aliikaribisha
kampuni hiyo kufanya ziara Tanzania mwezi Novemba 2025 ili kuitambulisha
teknolojia hiyo na kuanza majaribio ya awali akielezea kwamba hii itakuwa ni
sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuongeza pato la taifa, kupambana
na umaskini, kuongeza ajira na uzalishaji na kuuza chakula nje ya nchi baada ya
nchi kufikia usalama wa chakula kwa asilimia 140.
0 Maoni