Umoja wa Ulaya (EU)
umetahadharisha kuhusu kasi ya kupungua kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro,
hatua inayotajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa mazingira na maisha ya jamii
zinazotegemea rasilimali za mlima huo.
Akizungumza jana Septemba 19,
2025 wakati wa ziara ya Waheshimiwa mabalozi wa Umoja wa Ulaya waliotembelea
Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Balozi wa Finland Nchini Tanzania. Mhe.
Theresa Zitting amesema hali ya kuyeyuka kwa barafu katika kilele cha Uhuru ni
ishara ya wazi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia.
“Ni jambo la kusikitisha kusikia
na kushuhudia jinsi barafu inavyopungua na namna hali hiyo inavyotarajiwa kuathiri
mtiririko wa maji na mfumo wa ikolojia katika maeneo ya chini ya mlima. Tatizo
hili halipo Tanzania pekee; hata nchini mwangu Finland tunashuhudia mabadiliko
ya joto,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizotolewa, takribani watalii 60,000 hutembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kila mwaka,
wengi wao ni kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo, viongozi hao
wameelezea hofu ya kupungua kwa barafu na mabadiliko ya tabianchi kunaweza
kudhoofisha kivutio hicho cha kimataifa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Katika mikakati yake ya
kimazingira, EU kupitia balozi wake hapa nchini Bi. Christine Grau alisema
wamejipanga kuendeleza ushirikiano na Tanzania kupitia sera za Green Deal
zinazolenga kufikia usawa wa sifuri wa kaboni na kutimiza malengo ya Mkataba wa
Paris.
Pia, EU imesisitiza dhamira yake ya kuisaidia Afrika
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi bila kuibebesha mzigo wa
uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na bara la Ulaya.
Aidha, Umoja wa Ulaya umesisitiza
umuhimu wa kulinda misitu ya Tanzania, ikiwemo kuongeza misitu ya kupandwa na
kudhibiti ukataji hovyo ili kudumisha mfumo wa ikolojia unaochangia kupunguza
hewa ya ukaa.
Kwa sasa, takribani asilimia 55
ya eneo lote la Tanzania limefunikwa na misitu, hali ambayo wataalamu wanasema
ni ngao muhimu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
EU imeahidi kuendelea
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika uhifadhi endelevu wa misitu,
maendeleo ya kilimo rafiki kwa mazingira, na kubadilishana teknolojia za
kukabiliana na changamoto za tabianchi.
“Tunachokiona hapa ni mfano wa
changamoto za kidunia zinazohitaji mshikamano wa kidunia. Mlima Kilimanjaro ni
urithi wa dunia, na jukumu la kuutunza ni letu sote,” alihitimisha Balozi huyo
wa EU.
Afisa Uhifadhi Mwandamizi ambaye
pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utalii KINAPA, Stephen Moshy, alisema ziara hiyo
imewapa nafasi ya kueleza fursa zilizopo katika hifadhi na jinsi jamii
zinazozunguka mlima huo zinavyonufaika na rasilimali zake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Amri Mtekanga, alisema mabalozi hao walipata
nafasi ya kujifunza kuhusu shughuli mbalimbali za utalii, ikolojia na usimamizi
wa mazingira katika hifadhi hiyo unaofanywa na TANAPA.
Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro
(KINAPA) imepokea ugeni wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya kutoka nchi 12, hatua
inayotajwa kuwa fursa kubwa kwa utalii na ushirikiano wa kimataifa na
utachagiza ongezeko la watalii katika hifadhi hiyo siku za usoni.
0 Maoni