Katika
juhudi za kuboresha upatikanaji wa maji safi, mitambo iliyofungwa Bukanga,
Musoma Mjini inazalisha lita milioni 36 za maji kwa siku, kiasi ambacho ni
kikubwa kuliko mahitaji ya kila siku ya Mji wa Musoma, uliopo mkoani Mara.
Ili
kuimarisha usambazaji wa maji, tenki kubwa lenye ujazo wa lita milioni tatu
limejengwa Mlimani Bharima, na MUWASA wanaendelea kusambaza maji ya bomba
katika jimbo la Musoma Vijijini.
Taaifa ya
Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo imesema tenki hilo litatumika
kusambaza maji ya bomba ndani na nje ya Mji wa Musoma. Serikali imeipa MUWASA
jukumu la kusambaza maji haya kwa vijiji jirani, ikiwemo vijiji vya Musoma
Vijijini na Butiama.
MUWASA
imepanga kusambaza maji kwenye kata nne za Musoma Vijijini, kwenye Kata ya
Etaro vijiji vitatu, Kata ya Nyegina vijiji vitatu, kata ya Nyakatende vijiji vinne
na Kata ya Ifulifu vijiji vitatu.
Taarifa
inasema hadi sasa, usambazaji wa maji ya bomba umefanikiwa kwenye baadhi ya
vijiji vya Kata ya Etaro (Busamba, Etaro, na Mmahare) na Nyegina (kijiji cha
Mkirira) ambapo kazi yakutandaza bomba kuu kuelekea Nyegina Senta inaendelea.
Aidha, imeeleza
taarifa hiyo kuwa katika Jimbo la Musoma Vijijini, vijiji 68 vinanufaika na
miradi ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria, ambapo vijiji 53 kati ya 68
(77.94%) tayari vinatumia maji ya bomba.
Miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, na baadhi ya vijiji vinafanyiwa kazi ya kuchimba visima virefu, hasa katika Kata ya Bugwema. Kazi hii inafanywa kwa ushirikiano kati ya RUWASA, MUWASA, na BADEA.
Wananchi wa
Jimbo la Musoma Vijijini na viongozi wao wote wameendelea kuishukuru Serikali chini
ya uongozi mzuri wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia
fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijijini vyao, ikiwemo
miradi ya maji safi na salama ya bomba, imemalizia taarifa hiyo.
0 Maoni