TANZANIA
inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa masuala ya nishati barani Afrika
utakaotafuta namna ya kukusanya dola za Marekani bilioni 190 ili zitumike
kufikisha umeme kwa wananchi milioni 300 barani humo ifikapo mwaka 2030.
Hatua hiyo
inatokana na mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kupeleka umeme vijijini na
vitongojini kwa kasi hali ambayo imezivutia taasisi za Benki ya Dunia na Benki
ya Maendeleo Afrika (AfDB) kuamua kufanya mkutano huo mkubwa ifikapo Januari,
2025.
“Wameridhishwa
na utendaji kwenye sekta ya nishati, wameridhishwa na mkakati wa Serikali wa
kupeleka umeme mpaka vijijini, siyo tu vijijini lakini mpaka kwenye kila
nyumba. Wameamua kuitisha mkutano mkubwa barani Afrika ambao utawakutanisha
wadau mbalimbali, taasisi za Kimataifa na taasisi zinazotoa mikopo kwa
wajasiriamali na makampuni ili waweze kuwekeza kwenye umeme.”
Hayo
yalisemwa Jumatatu, Septemba 23, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye
mkutano wa kujadili ajenda ya upatikanaji wa nishati Afrika ulioandaliwa na
taasisi ya Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP) jijini New
York, Marekani.
Akizungumza
na washiriki wa mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za taasisi ya Rockefeller,
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa baraka zake
ili Tanzania iwe mwenyeji wa mkutano huo.
Alisema
mkutano huo ambao utaendeshwa kwa pamoja baina ya Benki ya Dunia, Benki ya ADB
na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, unatarajiwa kuwaunganisha viongozi wa dunia,
waatalamu wa kutoka viwandani, asasi za kiraia katika kutafuta namna ya
kuwezesha upatikanaji wa nishati za uhakika, teknolojia bora za nishati safi na
sera endelevu.
“Ninaipongeza
Serikali ya Norway na taasisi ya Rockefeller kwa kuamua kuunga mkono jitihada
za Benki ya Dunia na ADB za kuhakikisha umeme unapatikana kwa watu milioni 300
ifikapo mwaka 2030. Mpango huu ni wa muhimu hasa kwa nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara ambako watu zaidi ya milioni 600 hawana fursa ya kupata umeme.
Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu kama hatutashughulikia kwa haraka
changamoto hii,” alisema.
Waziri Mkuu
alizishukuru Benki ya Dunia na AfDB kwa ahadi yao kuwa wataendelea kushirikiana
na Serikali ili kufanikisha mkakati wa Tanzania wa kupeleka umeme kila nyumba
uwe umekamilika ifikapo 2030.
Mapema, Rais
wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina alisema wanawake
milioni 900 wanataabika kwa kukosa nishati safi ya kupikia na kila mwaka ilhali
upishi unapaswa uwe ni wa staha. “Wanawake milioni 130 wanatakiwa wawe
wamefikiwa na huduma hii kila mwaka. “Tunapoteza wanawake na watoto wengi kwa
sababu ya kukosa huduma hii.”
Dkt. Adesina
alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vema sekta ya nishati
na hasa uzalishaji wa nishati safi ya kupikia na kwamba anataka kuona ifikapo
mwaka 2030, malengo ya kuhama kutoka kupikia kuni na mkaa kwenda nishati safi
yawe yametimia.
Wakati huo huo,
Rais wa Liberia, Joseph Boakai ambaye pia alishiriki kikao hicho, alisema umeme
ni suala la muhimu sana kwenye maisha ya mwanadamu na linapaswa kupewa
kipaumbele kikubwa kwani bila umeme hakuna maendeleo.
Alisema
nchini Liberia ni asilimia ndogo tu ya nchi hiyo ndiko wanapata umeme na tena
kwenye maeneo ya mji mkuu. “Nchini Liberia, maeneo mengi ya vijijini yako
gizani, na maeneo yenye umeme hayafikii asilimia 20. Unawezaje kupanga ajenda
za maendeleo kama hauna umeme? Unawezaje kwenda hospitali wakati hakuna umeme?
Hili ni suala nyeti na hatupaswi kuendelea kulisubiria kwa muda mrefu,”
alisisitiza.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu alisema Tanzania inaungana na mataifa mengine ambayo
yanaunga mkono mkakati wa hatuna haja ya kumuacha mtu nyuma katika suala zima
la ujenzi wa kesho iliyo bora kwa vijana.
Ametoa kauli
hiyo wakati akichangia mada kwenye mjadala wa The Future Starts Now uliokuwa
sehemu ya kuhitimisha Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Kujadili Hatma ya Siku Zijazo (Summit of the Future) ulioanza juzi kwenye makao
makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.
“Kuna haja
ya kuwaandaa vijana wetu ili wawe watu bora. Tuanze nao leo, tusisubiri kesho.
Tuwape fursa za kushiriki kwenye kilimo, mifugo, uvuvi na uchumi wa bluu kwa
ujumla wake.”
Waziri Mkuu
ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo atashiriki
ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79).
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kitaifa,
Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila
Mkumbo na Waziri wa Afya wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wengine wa
Serikali.
0 Maoni