Viongozi wa Kanisa ongezeni juhudi kusimamia shule za jumapili- Mhe. Kitandula

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amewataka viongozi wa Kanisa kuweka mkazo kwenye kuimarisha shule za Jumapili kwa ajili ya kuimarisha misingi ya dini na malezi bora kwa watoto kwa kuwa dunia ya sasa mmonyoko wa maadili umekuwa mkubwa na unadhoofisha misingi ya maadili kwa taifa.

Mhe. Kitandula Ameyasema hayo alipokuwa akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Mazishi ya Askofu Mstaafu Joseph Mathayo Jali wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Mashariki wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Aidha, Mhe. Kitandula akitoa Salam maalum za Serekali amemzungumzia Askofu Mstaafu Jali kuwa  alikuwa mtu wa kipekee ambaye maisha yake yalionyesha mfano halisi wa kiongozi wa kiroho aliyempenda Mungu na wanadamu. Maneno yake yalijaa hekima, na matendo yake yameandika historia katika huduma na mapenzi kwa jamii. Muda wote wa utumishi wake, aliutumia katika maisha ya watu, na hiyo inathibitisha dhati ya uongozi wake wa kiroho kwenye jamii.

Vilevile aliongeza kuwa Askofu Mstaafu Jali alikuwa muumini mkubwa wa utunzaji wa Mazingira kwa kuhimiza upandaji wa miti, utunzaji wa mazingira na uoto wa asili kila alipokuwa akienda kuanzisha huduma za kiroho kwenye maeneo mbalimbali. 

Aidha, Mhe. Kitandula alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa Kanisa na waumini wote nchini kumuombea Mhe. Rais na wasaidizi wake wote ili waliongoze taifa letu kwa haki na kweli; na hatimae amani na upendo uendelee kutamalaki nchini. 

Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dk. Gehaz Malasusa wakati akimkaribisha Naibu Waziri Kitandula aliwataka waumini kufanya rejea ya Maisha ya Askofu mstaafu Jali aliyoishi hapa duniani yatumike kuwaunganisha wakristo kuwa kitu kimoja na kuishi kwa Amani, ushirikiano na kuwa watu wa kusamehe ili kujiwekea hazina iliyobora mbinguni.

Baba Askofu Mstaafu Joseph Jali alifariki tarehe 14/8/2024 ambapo wakati wa uhai wake alihudumu katika nyadhifa mbalimbali mpaka alipowekwa wakfu tarehe 21/11/1993 kuwa askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki hadi alipoostaafu Februari mwaka 2001.

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) akiweka shada la maua katika kaburi la Askofu Mstaafu Joseph Mathayo Jali wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Mashariki wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Na. Anangisye Mwateba- Lushoto Tanga

Chapisha Maoni

0 Maoni