Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amebainisha kuwa
Tanzania iko tayari kuvutia Wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kupitia
Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, unaotarajiwa
kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2024.
Amebainisha hayo leo Agosti 21, 2024, katika Hoteli ya
Johari Rotana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika hafla ya Uzinduzi
wa Mkutano huo.
Waziri Mavunde amesema kuwa Mkutano huo utaleta pamoja wadau
wa kimataifa katika Sekta ya Madini, Wawekezaji, Watafiti wa Madini,
Wachimbaji, Wawakilishi wa Serikali, Viongozi kutoka Mataifa ya kigeni,
Wawakilishi na Mabalozi wa nchi mbalimbali kwa pamoja wakilenga kujadili fursa
za kipekee za Uwekezaji katika uongezaji thamani madini, uchimbaji na hususan
wakati huu ambapo mahitaji ya madini muhimu yanaongezeka duniani.
“Ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba
madini yote yanayochimbwa hapa nchini ili kuongeza mchango wa Sekta katika Pato
la Taifa, kulinda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea ukuaji
wa teknolojia katika Sekta, kuchochea maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla,"
amesema Waziri Mavunde.
Akiweka msisitizo kwenye kaulimbiu ya mkutano huo,
"Uongezaji Thamani Madini kwa
Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi Waziri Mavunde amesema Mkutano huo utakuwa
jukwaa muhimu la majadiliano ya kina yatakayotoa mwelekeo mpya kwa sekta ya
madini nchini, huku ukiibua fursa mpya za uwekezaji na uhamishaji wa
teknolojia.
Vilevile, Waziri Mavunde amesema kuwa, Mkutano huo pia
unatarajiwa kuwa fursa ya kipekee kwa washiriki kufahamu Sera za Madini za
Tanzania, vivutio vya uwekezaji, na mipango ya serikali ya kuboresha mazingira
kwa ajili ya kuvuna madini kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri
Mbibo amesema kuwa Mkutano huo utakuwa msingi wa kujenga uwezo na uhamishaji wa
teknolojia kupitia majadiliano ya kina ya kitaalamu na mawasilisho ambayo
yatatoa mwelekeo mpya kuhusu jinsi ya kuboresha sekta, pamoja na kutafuta fursa
mpya za kuongeza thamani ya madini.
“Mkutano huu pia utatoa fursa za uwekezaji kwa kuvutia zaidi
kampuni za utafiti, uchimbaji, usindikaji na uongezaji thamani madini, na watoa
huduma ili kuchimba na kuongeza thamani madini muhimu na vito vinavyopatikana
Tanzania,” ameongeza Mbibo
Naye, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania Mhandisi
Benjamin Mchwampaka amesema kuwa wao kama Chemba ya Migodi wanaishukuru Wizara
ya Madini kwa kuwachagua kushirikiana kwa pamoja katika kuandaa mkutano huo.
“Sisi ndio sauti ya Wawekezaji katika Sekta ya Madini hapa
nchini, tunaamini kuwa mkutano huu utatuongezea ufanisi katika namna ya
uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini,
pia kupitia ushirikiano huu tunaamini tutakuwa na Mkutano mzuri mwezi Novemba
2024” amesisitiza Mhandisi Mchwampaka.
Pia, Mkutano huo utaambatana na Usiku wa Madini ambayo ni Maonesho ya Vito yenye lengo la kutangaza utajiri mkubwa wa Tanzania katika madini ya vito sambamba na tukio la kuwatambua Kampuni na Wachimbaji waliofanya vizuri kwa kipindi kilichopo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara, watendaji wa taasisi za Wizara, Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nje zao nchini, wamiliki wa Leseni kubwa za uchimbaji Madini,wamiliki wa leseni za kati, watoa huduma migodini na wafanyabiashara wa madini, taasisi za fedha na wadau mbalimbali wa madini.
0 Maoni