Mtangazaji nguli, na mwandishi wa habari mashuhuri Africa Mashariki na Kati aliyekuwa akitangaza kipindi cha Dira ya Dunia katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambaye kwasasa anafanya kazi na Redio/TV ya Crown FM/TV iliyopo nchini, Salim Kikeke amesema uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini - TAWA katika Tamasha la Kizimkazi umekuwa chachu ya kuchagiza na kulipa hadhi tamasha hilo kutokana na Taasisi hiyo kuwapeleka wanyamapori hai ambao wamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wengi wanaotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kikeke ameyasema hayo leo Agosti 21, 2024 alipotembelea
banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kufika katika bustani ya wanyamapori
hai ambapo alipata fursa ya kujionea aina mbalimbali za wanyamapori wakiwemo
Simba, Chui, Fisi, Chatu, Pundamilia na spishi za aina tofauti za ndege nyuni.
"Niko hapa Kizimkazi kwa ajili ya Tamasha la Kizimkazi
na nimefurahi sana kutembelea banda hili la TAWA...kuna mabanda mengi sana
lakini TAWA wameweza kuleta kivutio cha kipekee kabisa, wameleta wanyama
mbalimbali na zaidi ni kuonesha hazina ya Taifa letu," amesema
"Nadhani kitu TAWA wanakifanya ni muhimu sana kuweza
kuja kutoa elimu na kufahamisha jamii yetu ya hapa hapa nyumbani lakini
vilevile watu wanaotoka nje ya Taifa
letu kufahamu maana halisi ya wanyama hawa, jinsi tunavyowatunza na jinsi
wanavyolisaidia Taifa letu kwa njia ya kipato kwahiyo pongezi nyingi sana kwa
TAWA kwa kile wanachokifanya uwepo wao nadhani umeongeza ile hadhi ya Kizimkazi,"
ameongeza na kusisitiza Kikeke
TAWA ni mojawapo ya Taasisi za Serikali zinazoshiriki katika Tamasha hilo kwa lengo la kutangaza fursa za utalii zilizopo katika maeneo yake ya kimkakati yaliyo chini ya usimamizi wake hususani ya ukanda wa Kusini Mashariki Kama vile Hifadhi za Selous, Kilwa, Pande (Dar es Salaam), Wamimbiki (Pwani/Morogoro) n.k ikiwa ni muendelezo wa kuunga mkono jitahada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotangaza vivutio vya Utalii wa nchi yetu kupitia filamu Maarufu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Na. Beatus Maganja- TAWA
0 Maoni