Meneja wa Viwango na Uhakiki, Wakala wa Vipimo Tanzania
(WMA), Magesa Biyani ametoa rai kwa wabunifu wa vipimo pamoja na teknolojia
mbalimbali zinazohusiana na uhakiki wa vipimo kuchangamkia fursa kwani sekta
hiyo inakua kwa kasi jambo linalokwenda sambamba na uhitaji wa vipimo vya
kisasa na teknolojia mpya za uhakiki wake.
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya
WMA kwa Wakufunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Akidadavua kuhusu uhakiki wa vipimo ambao ni jukumu la
msingi la WMA, Biyani amesema Wakala hiyo inaendelea kuongeza wigo wa utendaji
kazi wake kwa kuzifikia sekta mbalimbali ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa
katika uchumi wa nchi.
Ametolea mfano wa baadhi ya sekta hizo kuwa ni pamoja na
umeme, gesi asilia, mafuta, maji, mawasiliano, usafiri na nyingine nyingi na
kufafanua kuwa tayari wamekwishaanza utekelezaji kwa baadhi yake, kazi ambayo
ni endelevu yenye malengo ya kuzifikia sekta zote zinazojihusisha na vipimo.
“Kutokana na kukua kwa kasi kwa sekta ya vipimo, natoa rai
kwa wasomi na wabunifu mbalimbali kubuni vipimo vya kisasa pamoja na teknolojia
mpya na rafiki kwa mazingira ya nchi yetu kwa ajili ya uhakiki wa vipimo,”
amesisitiza.
Biyani amempongeza mmoja wa Wahadhiri wa DIT, Georgia Rugumira
anayeendelea na zoezi la kubuni Mzani utakaotumika kupima bidhaa mbalimbali.
Amemkaribisha kutembelea Wakala wa Vipimo ilia pate mwongozo
na ushauri zaidi kwa ajili ya kufanikisha ubunifu wake.
Aidha, amewakaribisha na kuwahamasisha Wahadhiri na wanafunzi
wa Chuo hicho kutembelea WMA ili kubadilishana uzoefu na kujifunza kwa vitendo
ili kupata wataalamu wabobevu katika sekta ya vipimo watakaotoa mchango mkubwa
katika kukuza uchumi wa nchi na wa mwananchi mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Viwanda na
Mwongozo wa Kazi kutoka DIT, Dkt. Sosthenes Karugaba ameishukuru WMA kwa kuona
umuhimu na kutenga muda wa kuwapatia wakufunzi wa chuo hicho elimu kuhusu
vipimo sahihi.
“Kwa niaba ya wakufunzi wenzangu, ninatoa shukurani za dhati
kwa WMA juu ya ugeni wenu hapa. Tumejifunza mengi kuhusu vipimo na tumepata
maarifa katika maeneo mbalimbali ya kiufundi. Tutaandaa utaratibu rasmi wa kuja
kuwatembelea huko WMA ili kujifunza zaidi. Tutakuwa mabalozi wazuri wa matumizi
sahihi ya vipimo katika jamii,” amesema.
Awali, akiwasilisha Mada kwa Wahadhiri hao wa DIT, Afisa
Vipimo kutoka WMA, Jadi Kijumu alibainisha kuwa Wakala hiyo iliyoanzishwa mwaka
2002, iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa na jukumu kuu la
kumlinda mlaji wa bidhaa na huduma kupitia matumizi sahihi ya vipimo.
Kwa upande mwingine, alisema WMA humlinda muuzaji wa bidhaa
na huduma kwa kuhakikisha anapata faida stahiki kulingana na mauzo ya bidhaa na
huduma anayotoa.
Wakala wa Vipimo imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu sahihi ya matumizi ya vipimo na kuwapa ushauri wa kitaalamu wadau mbalimbali ili kuwajengea ufahamu na kutatua changamoto mbalimbali za masuala ya vipimo.
Na. Mahamudu Jamal-
WMA
0 Maoni