Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Mkoa wa Dodoma wametakiwa kupunguza kutoa vibali vya kukata miti kwaajili ya kuchoma Mkaa kwani Nishati ya Mkaa inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uharibifu wa mazingira na hivyo kudhoofisha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Haya yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dr. Philip Isdor Mpango akiwa kwenye ziara ya siku tatu ya mkoa
wa Dodoma ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo. Aidha
Mhe. Mpango amewaasa Wananchi wa Wilaya za Chamwino na Bahi kuacha kuharibu
mazingira kwa kukata miti hovyo pamoja na kutoharibu maeneo oevu ambayo mengi
ni vyanzo vya maji.
Mhe. Mpango ameelekeza elimu itolewe kwa wananchi ili waweze
kutumia nishatI safi ambayo ni mbadala kwa ajili ya kupikia na kusisitiza
utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa wingi ili kupunguza changamoto ya
mabadiliko ya tabia nchini.
Katika ziara hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Pindi
Hazara Chana amewakilishwa na Naibu Wazili wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan
Kitandula.
Mhe. Kitandula alipopewa nafasi ya kusalimia wananchi
alisema kuwa Wizara ya Maliasili itaendelea kusimamia na kulinda maliasili
zilizopo nchini sambamba na kuwalinda wananchi wanaokabiliwa na changamoto ya
wanyama wakali na waharibifu.
Vilevile Mhe. Kitandula aliongeza kuwa wizara Itaendelea kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhimiza utunzaji wa misitu na upandaji wa miti kwenye maeneo yaliyo athirika kutokana na uharibifu wa mazingira.
Na. Anangisye Mwateba- Dodoma
0 Maoni