Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha vikundi 3,963 vya malezi chanya kwa lengo la kutumika kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii katika kukabiliana na changamoto za malezi nchini.
Hayo yamebainishwa mkoani Songwe na Mkurugenzi Msaidizi
Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Asha Shame wakati akifungua mafunzo ya wajibu wa
wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya familia kwa Maafisa Maendeleo ya
Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Elimu kutoka Ofisi ya Mkoa wa Songwe,
Halmashauri za Ileje, Mbozi na Tunduma kwa lengo la kuwawezesha maafisa hao
kutoa elimu hiyo kwa jamii Agosti 19, 2024.
Asha amesema Serikali imeendelea kutumia majukwaa tofauti
yakiwemo ya viongozi wa dini na waandishi wa habari katika kutoa elimu ya
wajibu wa wazazi na walezi katika malezi ya watoto na familia.
"Jumla ya viongozi wa dini 109 kutoka katika madhehebu
ya Kikiristo na Kiislamu (TEC, CCT, BAKWATA, CPCT na SDA) ambapo jumla ya
waumini 35,520 wameweza kufikiwa na elimu hii. Jitihada nyingine ni kuanzishwa
kwa vituo vya kulelea Watoto mchana vya kijamii ambapo tayari vituo 255
vimeshaanzishwa,” amesema Mkurugenzi Asha.
Ameongeza kupitia tafiti iliyofanyika mwaka 2015 ilibainika
kuwa wazazi wengi hasa wa kiume wamekuwa hawawajibiki katika malezi ya watoto
na kupelekea jukumu hilo kubebwa na wazazi wa kike katika maeneo yote ya mjini
na vijijini.
Aidha, amesema elimu ya malezi kwa wazazi ilionekana kikwazo
katika suala la malezi makuzi na maendeleo ya mtoto ikiwemo lishe bora, afya,
malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji na ulinzi na usalama wa mtoto.
Kupitia mafunzo hayo washiriki wanategemewa kutoka na mbinu
mbalimbali zitakazowawezesha kuzifikia jamii kuanzia ngazi ya kaya pamoja na
wadau muhimu katika malezi ya watoto, kupata elimu ya mnyororo chanya wa malezi
ya watoto kuanzia kipindi cha utungaji wa mimba mpaka vijana balehe na
kuandaliwa kwa mpango kazi wa Mkoa wa Songwe kuhusu utekelezaji wa Mwongozo wa
Wajibu wa Wazazi na Walezi katika malezi na Matunzo ya Familia.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Interfaith Patership
(TIP) Asina Shenduli akitoa salaam za Shirika hilo amesema kwa kushirikiana na
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na
shirika la UNICEF wameahidi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu
ya malezi chanya kwa watoto na familia inatolewa kwa jamii, hususan katika
ngazi za chini.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Songwe
Menrad Dimoso akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa amesema Ofisi ya
Mko wa Songwe itaendelea kusimamia utekelezaji wa mafunzo kwa maafisa hao ili
jamii waweze kupata elimu hiyo ili kusadiaia wazazi na walezi kujua wajibu wao
katika malezi na magtunzo ya familia kwa ustawi wa jamii na taifa.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Interfaith Patership (TIP) NA UNICEF wanaendesha mafunzo kwa Maafisa wa Serikali kwa kada za Elimu, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya wajibu wa mzazi na mlezi katika malezi na matunzo ya familia.
0 Maoni