MNH-Mloganzila yapokea msaada wa vifaa tiba vya kuhudumia watoto wachanga

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) chini ya mradi wa NEST 360 ambao una lengo kuboresha huduma kwa watoto wachanga wanaohudumiwa kwenye kitengo cha uangalizi maalum kwa watoto wachanga chini ya siku 28.

Msaada uliotolewa ni pamoja na mashine za tiba mwanga (phototherapy machines), mashine za kufuatilia joto kwa watoto wachanga na vifaa tiba vingine ambavyo vinatumika kutoa huduma katika kitengo hicho ambavyo jumla yake vina gharama ya takribani TZS 53 Mil.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba Shirikishi. Dkt. Lulu Sakafu ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo na kuongeza kuwa vitasaidia kuboresha huduma za watoto na hivyo wameienzi falsafa ya huduma bora kwa mteja kwa vitendo.

"Tunawashuru (NEST360) kwa kutambua umuhimu wa watoto wachanga kwakuwa wao ni taifa la kesho, msaada huu utasaidia katika kuimarisha kitengo cha kuhudumia watoto wachanga wanaozaliwa chini ya siku 28 (NICU)," amesema Dkt. Lulu.

Kwa upande wake Mratibu wa Uboreshaji Endelevu wa Huduma za Afya kupitia mpango wa NEST360 unaotekelezwa na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) Dkt. Robert Tillya, amesema kuwa wataendelea kutoa msaada kadri itakavyowezekana ili kuendelea kuunga mkono juhudi za hospitali za kuboresha huduma na kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Naye. Daktari Bingwa wa Watoto MNH-Mloganzila ameeleza kuwa asilimi 80 ya watoto wanaozaliwa chini va siku 28 wanapata manjano hivyo mashine hizo zitaongeza idadi ya mashine na kuwezesha watoto wengi kuhudumia kwa wakati mmoja.

Chapisha Maoni

0 Maoni